Aliyekuwa mgombea urais wa Chadema chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa amesema kusakamwa kwa maneno ya kejeli, vijembe na vitisho, kuitwa gamba na fisadi ndani ya CCM ndiko kulikomfanya kukihama chama hicho na kwenda upinzani.
Lowassa aliyekuwa na nguvu ya ushawishi ndani na nje ya CCM, alihamia Chadema baada ya jina lake kukatwa katika mchakato wa kumsaka Rais wa Tanzania, katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana.
Akizungumza katika mahojiano maalumu ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Lowassa alisema licha ya kuitumikia CCM kwa zaidi ya miaka 30 tangu mwaka 1977, chama hicho kiliamua kutumia watu kumsakama kwa kila aina ya maneno jambo lililomfanya achoke na kuamua kuondoka.
“Nakifahamu Chama cha Mapinduzi, nakiheshimu kwani ndicho kilichonilea, lakini, kwa hali tuliyokuwa tumefikia, inafika mahali unasema imetosha,” alisema Lowassa.
Alitaja sababu nyingine iliyomfanya kuihama CCM kuwa ni kutaka mabadiliko na aliamini mabadiliko ya kweli yatapatikana nje ya chama hicho tawala na akisema hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alisema mabadiliko yatatafutwa hata nje ya CCM.
Alisema kwa namna yoyote, kamwe hana mpango na hawezi kurudi CCM na akasema jukumu lililopo mbele yake kwa sasa ni kuijenga Chadema ambayo yeye ni Mjumbe wa Kamati Kuu.
“Sina mpango na wala siwezi kurejea CCM, mimi ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, na jukumu lililoko mbele yangu ni kukijenga na kukiimarisha chama changu hiki kiwe imara tangu katika ngazi ya matawi,” alisema na kuongeza kuwa kazi iliyoko mbele yake sasa ni kukiimarisha chama hicho na wamejipanga kuzunguka nchi nzima kufanya kazi hiyo pamoja na kuwashukuru nwananchi kwa imani waliyoionyesha kwake na chama chake.
Lowassa alidai kuwa kama si kura kuchakachuliwa, alikuwa na nafasi kubwa ya kushinda kwa sababu wananchi walishaichoka CCM na wakawa wanataka mabadiliko.
Alisema kazi nyingine kubwa waliyonayo sasa ni kuhakikisha Katiba Mpya inapatikana na Tume ya Uchaguzi inaundwa upya kwani iliyopo si huru hata kidogo.
Alisema kama isingekuwa busara na ukomavu waliouonyesha Ukawa, basi hata hali ya siasa Tanzania Bara isingelikuwa shwari kama ilivyo sasa.
“Mara baada ya matokeo ya uchaguzi, niliwashauri vijana watulie, wasifanye fujo, nashukuru walinisikiliza.”
Alisema katika uchaguzi huo yeye na Ukawa walishinda kwa kishindo isipokuwa matokeo yalivurugwa makusudi ili CCM iendelee kubaki madarakani.
“Nilishinda na Ukawa ilishinda, kilichotokea kura zilichakachuliwa kwa kiasi kikubwa… wao wanajua, Watanzania wanajua na kila mtu anajua, tulishinda kwa kura nyingi sana na tulipokonywa ushindi wetu,” alisema.
Vijana wa Chadema kukamatwa
Alisema miongoni mwa mambo yanayomuumiza na ambayo hatayasahau katika uchaguzi huo ni kitendo cha polisi kwa maagizo ya watendaji wa Serikali kuwakamata vijana waliokuwa wanakusanya matokeo na kuwadhalilisha ikiwa ni pamoja na kuwaweka mahabusu.
Alidai kuwa kitendo cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuvuruga kituo chao walichokuwa wakijumuisha matokeo na kuacha kile cha CCM kilikuwa kibaya na kilichoonyesha wazi kuwa hawakuwa tayari kukubali kuona wakishindwa.
Alisema: “Ni aibu kubwa kwa Serikali kuwaumiza na kuwaweka ndani vijana wadogo wasiokuwa na hatia eti kwa sababu tu walikuwa wakiunga mkono mabadiliko."
Uhuru wa NEC
Lowassa alisema miongoni mwa mambo yanayozorotesha chaguzi nchini ni NEC ambayo alisema siyo huru na badala yake ni chombo kinachotumika na watawala.
Alisema chombo hicho hakitendi haki na kwamba ingekuwa mamlaka yake baada ya uchaguzi kwisha angekiondoa madarakani.
Alisema wakati umefika kwa Watanzania kuungana kudai Katiba Mpya na tume huru ya uchaguzi kwa maelezo kuwa bila Katiba mpya na tume huru kamwe hakuwezi kufanyika uchaguzi ulio huru na wa haki.
Demokrasia bungeni
Akizungumzia mwenendo wa Bunge, alisema linakwenda vizuri lakini ni mapema kulizungumzia kwa sasa.
“Katika Bunge hili wameingia vijana madhubuti bungeni, lakini hatua ya Serikali kuzuia Televisheni ya Taifa (TBC) kurusha matangazo ya Bunge moja kwa moja, hiyo ni dalili ya kuminya demokrasia.”
Alisema ni aibu kubwa kwa Serikali kutumia polisi kuingia ndani ya Bunge badala ya kujenga hoja na akasema hali hiyo ikiachwa ikaendelea italitia aibu Taifa.
Alisema moja ya mambo yaliyohimizwa na ambayo Watanzania waliachiwa na Mwalimu Julius Nyerere ni utaratibu wa kujenga hoja na kutumia nguvu ya kushinda na akaongeza kuwa kitendo cha polisi kuingia na kupiga wabunge ni kuminya na kudidimiza demokrasia.
“Tanzania tunasifika duniani kote kwa kuheshimu na kufuata demokrasia, lakini Serikali imeamua kutumia polisi kuminya demokrasia, hii ni aibu kubwa kwa Taifa… Watanzania tukiacha demokrasia ikaminywa tutalitia aibu Taifa,” alisema.
Shukrani kwa Watanzania
Lowassa anasema licha ya kupokonywa ushindi, anajivunia mafanikio makubwa aliyoyapata kutoka kwa Watanzania walio wengi ambao walimuamini na kumuunga mkono.
“Watanzania waliniunga mkono kwa wingi sana, hali ile ilinipa faraja kubwa…nilifarijika pia nilipowaomba watulie wakanielewa na kutulia… nawashukuru sana Watanzania walionielewa na kutulia,” alisema.
Alitoa wito kwa Watanzania kuilinda amani ya nchi huku akisema anasubiri Rais Magufuli kutimiza siku 100 ndipo atoe tathmini yake kuhusu utawala wake.
“Marais wanapimwa kwa siku 100, nasubiri siku hizo, nitasema.”
Hali ya kisiasa Zanzibar
Akizungumzia hali ya kisiasa ya Zanzibar na uamuzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), kutangaza kurejewa uchaguzi upya, Lowassa alisema suala hilo ni zito na gumu na linahitaji maombi maalumu na umakini wa hali ya juu katika kulitatua.
Alitoa wito kwa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa CCM na Rais Magufuli kulishughulikia suala hilo mapema kabla ya Machi 20.
“Wasikubali tufike pabaya. Bado naamini tunaweza kulimaliza kwenye meza,” alisema na kuongeza:
“Nawasihi sana viongozi hawa wasilipuuze hili suala, jambo hili likiendelea litaleta shida kubwa kwa nchi yetu, magaidi wanaweza kulitumia na kuleta madhara makubwa, wasisubiri kufika pabaya, waanze kulishughulikia sasa.”
Alitoa wito pia kwa wanaoshughulikia suala hilo kuvishirikisha na vyama vingine badala ya kulifanya kuwa ni suala la CCM na CUF pekee.
Alisema ni imani yake kuwa Watanzania ni wamoja na hakuna mtu wa kuwagawa kwa namna yoyote na kuwa wasikubali uchaguzi huo wa marudio kuwa sababu ya kuivuruga amani ya nchi
No comments:
Post a Comment