Ezekiel Maige Atajwa Ufisadi Ngorongoro - LEKULE

Breaking

24 Feb 2016

Ezekiel Maige Atajwa Ufisadi Ngorongoro


Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii katika serikali ya awamu ya nne, Ezekiel Maige, jana alitajwa katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Bernard Murunya  ambaye ameshitakiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi.
Katika kesi hiyo, Maige anadaiwa kulipiwa nauli ya safari ya nje na mamlaka hiyo kwa idhini ya Murunya, ambaye sasa ni Mbunge wa Afrika Mashariki. 
Shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, Sezari Semfukwe, alidai kuwa Murunya na aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Mamlaka hiyo, Shad Kiambile, waliidhinisha malipo ya dola 66,890. Alidai kuwa fedha hizo zilikuwa kwa ajili ya safari ya Maige na msaidizi wake aliyetajwa kwa jina la E. Muyungi na Murunya mwenyewe.
Semfukwe, ambaye ni Kaimu Mhasibu Mkuu wa mamlaka hiyo, alidai kuwa Murunya na Kiambile, ndio walioidhinisha madokezo kwa ajili ya malipo hayo. 
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Hamidu Sembano, akisaidiana na Rehema Mteta, mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Patricia Kisinda, Semfukwe alidai kuwa utaratibu wa maombi ya safari, unatokana na maelekezo ya mkuu wa idara na kujaza fomu inayoonyesha anakwenda wapi na kwa muda gani.
Sambamba na hilo, alidai kuwa aina zingine za safari zinahusisha watu wa nje ambao, si waajiriwa wa NCAA kwa dokezo la mkuu wa idara au shirika.
Alidai kuwa alitoa hundi ya malipo namba 309/0238 ya Septemba 9/2011, ambayo ilikuwa na dokezo la safari kutoka kwa Murunya kwenda kwa Mkuu wa Kitengo cha Fedha. Pia  alitoa hundi ya malipo nyingine iliyokuwa ikionyesha imelipwa dola zaMarekani  66,890 kwa kampuni ya Wakala wa Usafirishaji ya Cosmas.
Aliendelea kudai kuwa hundi za malipo namba 310/0379 ya Oktoba 29, 2011 na ankara namba 5609 ya Septemba 7,  2011 zililipwa kwa Antelope Tours & Traveling kwa ajili ya tiketi za Murunya, Muyungi na Maige kwa malipo ya dola za Marekani 66,890 (zaidi ya Sh. milioni 133).
Shahidi hiyo alidai kuwa kumbukumbu ya kitabu cha malipo ya hundi inaonyesha hundi namba 002758 na 002755 za Septemba 9,  2011 zililipwa kwa kampuni ya Cosmas Travelling Agent na zilitiwa saini na Kiambile na Murunya.
Hata hivyo, wakati shahidi huyo akitoa vielelezo hivyo mahakamani hapo ili vitumike kama ushahidi, malumbano ya kisheria yaliibuka baina ya mawakili wa pande zote.
Malumbano hayo yaliibuka baada ya upande wa washtakiwa, ukiongozwa na wakili Amani Mirambo, kutaka kujua ni vielelezo vingapi au vya aina gani ambavyo upande wa mashtaka unavileta.
Hatua hiyo ilisababisha malumbano ya kisheria hivyo kumfanya hakimu kuahirisha kesi kwa dakika 10. Baada ya muda huo, alirejea mahakamani baada ya dakika hizo na kuwahoji.
Baada ya kuhoji pande zote mbili, kutokana na malumbano ya kisheria, Hakimu alikatizwa na Wakili wa Serikali Hamidu Simbano, aliyemwomba  kuahirisha kesi hiyo na kutaja tarehe nyingine ya  washtakiwa kusomewa maelezo yao ya awali.
Awali, Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Rehema Mteta, aliwasomea maelezo ya awali juu ya tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka yaliyosababisha mamlaka hiyo kupoteza dola 66,890 (Sh. 133,780,000).

Mteta aliwataja washitakiwa, mbali na Murunya na Kiambile, kuwa ni Meneja Utalii wa mamlaka hiyo, Veronica Funguo na Salha Issa ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Cosmas Travelling Agent.

No comments: