Dk. Magufuli Amtumia Salamu Za Rambirambi Mkuu Wa Mkoa Wa Tanga Kufuatia Ajali Vifo Vya Watu 11 - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Friday, 12 February 2016

Dk. Magufuli Amtumia Salamu Za Rambirambi Mkuu Wa Mkoa Wa Tanga Kufuatia Ajali Vifo Vya Watu 11Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bi. Mwantumu Mahiza, kufuatia vifo vya watu 11 waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyosababishwa na Basi la Kampuni ya Simbamtoto kugongana uso kwa uso na Lori lililobeba mchanga katika eneo la Pandamlima, Wilaya ya Muheza Mkoa wa Tanga.

Ajali hiyo imetokeo leo tarehe 11 Februari, 2016 majira ya saa 1:15 asubuhi katika eneo hilo lenye mteremko, ambapo basi la Kampuni ya Simbamtoto lilikuwa likisafiri kutoka Tanga kwenda Dar es salaam na Lori lililokuwa limebeba mchanga, lilikuwa likielekea kiwanda cha saruji cha Tanga.

Rais Magufuli amewapa pole Ndugu, Jamaa na Marafiki wote waliofikwa na msiba huo na amewataka kuwa wavumilivu na wastahimilivu katika kipindi hiki kigumu.

"Nimepokea taarifa ya vifo hivi kwa mshituko mkubwa, na kupitia kwako Mkuu wa Mkoa wa Tanga, napenda kuwapa pole nyingi wote waliofikwa na msiba huu mkubwa na naungana nanyi katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo" alisema Rais Magufuli.

Dkt. Magufuli amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema pepo, na amewapa pole majeruhi wote 21 walioumia katika ajali hii.

Aidha, Rais Magufuli amewakumbusha watumiaji wote wa barabara hususani madereva wa vyombo vya moto, kuwa makini watumiapo barabara kwa kuzingatia sheria zote zinazosimamia usalama barabarani ili kuepusha ajali.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam.
11 Februari, 2016
Post a Comment