CRDB Yawatoa Hofu Wateja Wake Baada Ya Serikali Kuagiza Akaunti za Taasisi zake Katika Mabenki ya Kibiashara Zifungwe - LEKULE

Breaking

2 Feb 2016

CRDB Yawatoa Hofu Wateja Wake Baada Ya Serikali Kuagiza Akaunti za Taasisi zake Katika Mabenki ya Kibiashara Zifungwe


(Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu serikali kuhamishia akaunti zote za mapato Benki Kuu. Kulia ni Mkurugenzi wa Hazina wa Benki ya CRDB, Alex Ngusaru na Mkurugenzi wa Masoko, Utafiti na Huduma kwa Wateja, Tully Mwambapa.)

****
SIKU chache baada ya Serikali kutangaza kuchukua hatua za kupunguza riba za mabenki kwa wananchi kwa kuagiza akaunti za mashirika na taasisi zake katika mabenki ya kibiashara zifungwe na kuhamisha fedha zilizopo katika akaunti hizo kwenda Benki Kuu ya Tanzania (BoT), benki ya CRDB imeunga mkono hatua hiyo.

Pia benki hiyo imewataka wananchi wasiwe na hofu juu ya mpango huo, kutokana na hofu iliyojengeka kwamba kuna hatari benki za kibiashara kufilisika nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk.Charles Kimei alisema uamuzi uliofanywa na Serikali utasaidia kukuza uchumi pamoja na kutambua fedha zake mahali zilipo.

Alisema Serikali ina haki na nia njema kwa kutaka akaunti hizo zifunguliwe BoT kwa kuwa zimekuwa zikifunguliwa kwenye mabenki makubwa ya kibiashara, huku baadhi ya Wakala wa ukusanyaji wa fedha wakishindwa kuzifikisha serikalini  kama inavyotakiwa.

Pia alieleza kuwa mfumo huo hauna utofauti na awali kwani utofauti utakuwepo kutokana na mashirika na taasisi kufungua akaunti BoT, ambapo lengo kubwa ni walaka wa Hazina kulenga kuboresha mapato ya serikali ammbayo yanaweza kutumiwa kwa namna mbalimbali.

“Mfumo huu…utakuwa hauna tofauti na ilivyo sasa kwa kuwa fedha zitakazokuwa zikiingizwa kwenye akaunti hizo ni zile zilizokuwa zikiingizwa kwenye benki awali, ili kupunguza kiwango cha riba,”alisema.

Pia alisema hofu nyingine inayojengeka kwa wananchi inatokana na mfumo huo kutotumiwa kwa muda mrefu na BoT, licha ya kuwa kuna baadhi ya nchi inatumia mfumo huo na hakuna madhara yoyote.

“Hivyo tunafikiri maamuzi hayo hayana athari zozote kwani nchi mbalimbali zimekuwa zikitumia mfumo huo ikiwemo Uganda, Rwanda na Kenya ila  kwetu unaonekana mgeni kutokana na kutotumika kwa muda mrefu,”alisema.

Pia Dk.Kimei alisema kuwa kutokana na uwepo wa mfumo huo,benki za kibiashara zitawakopesha zaidi sekta binafsi, ikiwa tofauti na malalamiko ya mwanzo kwamba Serikali inapata manufaa kutokana na kukopeshwa zaidi.

“Hii itasaidia hata wananchi wa kiwango cha chini kuchukua mikopo kutokana na riba kuwa ndogo, ambapo hata wananchi wa chini wataweza kuchukua mkopo, ikiwa tofauti na awali wananchi wanashindwa kuchukua mikopo kutokana na riba kuonekana kuwa juu zaidi ya asilimia 10,”alisema.

Mbali na hilo, pia Kimei alisema endapo riba ikiwa inapungua itasaidia kukuza uchumi kutokana na wananchi wengi wa hali ya chini kuchukua mikopo.

No comments: