Penny mara baada ya kushinda medali katika mashindano ya Olimpiki
Muogelaji
nyota wa zamani wa dunia na mshindi wa medali ya dhahabu ya michezo ya
Olimpiki kwa upande wa wanawake, Penelope “Penny” Heyns wa Afrika Kusini
ataendesha mafunzo ya siku mbili ya kuogelea kwa makocha wa klabu
maarufu ya mchezo huo hapa nchini, Dar Swim Club.
Penny
ambaye ni bingwa wa kihistoria wa michezo ya Olimpiki kwa staili ya
‘Breastroke’ atawasili nchini Alhamis akitokea Afrika Kusini tayari
kuendesha mafunzo hayo kwa makocha watano wa klabu hiyo. Katibu Mkuu wa
Dar Swim Club, Inviolata Itatiro alisema jana kuwa maandalizi
yamekamilika na klabu yao itagharimia mafunzo hayo kwa lengo la
kuboresha viwango vya wachezaji wao na makocha kwa ujumla.
Inviolata
alisema kuwa makocha wao watakaoshiriki katika kozi hiyo kuwa ni
Michael Livingstone, Ferick Kalengela, Radhia Gereza, Kanisi Mabena,
Adam Kitururu, Simon Ngoya na Salum Mapunda. Alisema kuwa makocha wao
wanasifa za ngazi ya juu ya ufundishaji wa mchezo huo, kutokana na kukua
kwa kasi kwa mchezo huo, wameona bora wapate mbinu za kisasa ili kwenda
na wakati.
“Makocha
wetu wote watano ni bora katika ufundishaji, waliwahi kupata mafunzo
Dubai, Marekani na nchi mbalimbali, lakini klabu imeona kuendelea kuwapa
mbinu zaidi ili kufikia malengo yetu ya miaka 10,” “Tunataka kuona kila
mtoto anacheza mchezo wa kuogelea, tulianza na watoto wadogo ambao kwa
sasa ni mastaa katika mchezo huo na kuweza kushinda medali mbalimbali
nje ya nchi,” alisema Inviolata.
Alisema
kuwa wao wameamua kupromoti mchezo wa kuogelea kwa vitendo ili kuona
siku moja watanzania wanafuzu kushindana michezo ya Olimpiki, Jumuiya ya
madola na mashindano ya dunia siyo kupata nafasi za upendeleo kama
ilivyo sasa. Alifafanua kuwa Penny alitwaa medali za dhahabu katika
mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika mjini Atlanta 1996 kwa mita 100 na
200 na wanaamini kuwa ujio wake utapandisha morali wachezaji wao na
makocha.
No comments:
Post a Comment