Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amesema Rais wa Burundi Pierre
Nkurunziza amekubali kufanya mazungumzo na upande wa upinzani kuumaliza
mzozo wa kisiasa nchini humo.
Ban
ambaye anafanya ziara yake ya kwanza Burundi tangu mzozo kuzuka nchini
humo mnamo mwezi Aprili mwaka jana, aliwasili jana alasiri na leo
amefanya mazungumzo na Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza mjini
Bujumbura.
Mkutano
huo unakuja baada ya Katibu huyo wa Umoja wa Mataifa kukutana na
viongozi wa vyama vya kisiasa na wa asasi za kiraia katika juhudi za
kuutafutia ufumbuzi mzozo wa Burundi ambao umedumu kwa miezi kumi.
Afisa
mmoja wa Umoja wa Mataifa amesema ziara ya Ban ni muhumu sana kwani
wanatumai atamshinikiza Rais Nkurunziza hatimaye kukubali kufanya
mazungumzo ya kina na yasiyo na masharti na wapinzani wake.
Ban Kuzuru Congo na Sudan Kusini(P.T)
Baada ya
mazungumzo hayo na Rais Nkurunziza, Ban ataizuru Jamhuri ya kidemokrasia
ya Congo na pia Sudan Kusini ambako kuna vita vya wenyewe kwa wenyewe
tangu mwezi Desemba mwaka 2013.
Ban
anatarajiwa kuzifufua juhudi zinazodhamiria kupatikana kwa suluhisho la
amani kwa mzozo wa kisiasa wa Burundi ambao ulichochewa na azma ya
Nkurunziza kugombea muhula wa ttau madarakani kinyume na sheria.
Serikali
ya Burundi inaonekana kulegeza msimamo wake dhidi ya wapinzani wake kwa
kukubali ujumbe wa viongozi wa nchi za Afrika wanaotarajiwa kuwasili
nchini humo baadaye wiki hii na kufutilia mbali waranti za kimataifa za
kukamatwa kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani.
Saa
chache kabla ya kuwasili kwa Katibu huyo wa Umoja wa Mataifa, watu
wawili waliuawa na wengine tisa walijeruhiwa katika mashambulizi
yaliyofanywa na washambuliaji waliokuwa katika pikipiki.
Meya wa
mji wa Bujumbura Freddy Mbonimpa ambaye ameyalaani mashambulizi hayo na
kuyataja vitendo vya kigaidi vinavyowalenga raia wasio na hatia amesema
mji huo umekuwa mtulivu kwa siku kadhaa zilizopita.
Mbonimpa
amesema washambualijai hao wamefanya mashambulizi hayo ili kudhihirisha
uwepo wao wakati ambapo Burundi inamtarajia mgeni muhimu.
Haijabainika
wazi ni nani hasa aliyehusika katika mashambulizi hayo ya maguruneti
ambayo yameongezeka katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita. Maafisa
wa usalama, waasi na upinzano wanalaumiana kwa mashambulizi hayo
yanayosababisha mauaji.
Wakati
huo huo, Ufaransa imewasilisha pendekezo katika Umoja wa Mataifa la
kupelekwa kwa askari wa Umoja huo nchini Burundi ili kutuliza ghasia.
Marais wa Afrika kuzuru Burundi
Ufaransa
inatumai kuwa pendekezo hilo litaidhinishwa kabla ya marais wa Afrika
wakiongozwa na Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma kuwasili Burundi siku ya
Alhamisi wiki hii kwa mazungumzo na Nkurunziza.
Balozi wa
Ufaransa katika Umoja wa Mataifa Francois Delattre amesema wanataka
kuchukua fursa ya kuwepo juhudi za pamoja za jumuiya ya kimataifa
kukomesha ghasia na kutafuta suluhisho la tija Burundi.
Mzozo huo
wa Burundi umesababisha vifo vya zaidi ya watu 400 na wengine zaiidi ya
240,000 wamelazimika kutorokea nchi nyingine. Maelfu ya watu
wamekamatwa na maafisa wa usalama wanashutumiwa kwa kuwaua watu kiholela
na kukiuka haki nyingine za kibinadamu.
Umoja wa
Mataifa umeonya kuwa Burundi iko katika hatari ya kutumbukia tena katika
vita vya wenyewe kama vilivyoshuhudiwa kati ya mwaka 1993 hadi mwaka
2005 ambapo kiasi ya watu laki tatu waliuawa.
Chanzo:DW
No comments:
Post a Comment