Waziri wa Ardhi , William Lukuvi Aagiza Kukamatwa kwa Watendaji wote Waliohusika na Kugawa Shamba la Ekari 3,500 Mkoani Morogoro. - LEKULE

Breaking

25 Jan 2016

Waziri wa Ardhi , William Lukuvi Aagiza Kukamatwa kwa Watendaji wote Waliohusika na Kugawa Shamba la Ekari 3,500 Mkoani Morogoro.



Serikali imeliagiza jeshi la polisi na taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa kuwakamata, kuwahoji na kuwafikisha mahakamani viongozi na watendaji wote hata kama wamestaafu madaraka yao, walio husika kutoa shamba la hekari 3,500,Morogoro.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, baada ya kutembelea kijiji hicho cha Mlilingwa,Ngerengere  kwa lengo la kujiridhisha juu ya mwenendo mzima wa utoaji wa eneo hilo ambao ulitiliwa mashaka na Rais.

Mhe. Lukuvi amelazimika kukagua sahihi za wana kijiji walio orodheshwa majina yao ambapo wengi wa waliohojiwa wamezikana sahihi hizo na kueleza kushangazwa na hali hiyo na hata baadhi ya majina yaliyotumika  sio ya wanakijiji wenzao na kudai katika kikao hicho hakuna mwenyekiti, mjumbe wala mtendaji aliyekuwa kwenye sakata hilo aliyehudhuria kikao hicho.

Mwakilishi wa kampuni ya Oxfod Trading LTD aliyehudhuria mkutano huo wa kijiji, ameonekana kushindwa kujieleza vyema pale alipokuwa akihojiwa maswali kwa madai bado ni mgeni katika kampuni hiyo na hakuwepo wakati wa mkutano wa kuidhinisha kutolewa kwa eneo hilo.

Baada ya kujiridhisha, waziri Lukuvi ameagiza mtu huyo kukamatwa na ofisa wa polisi ili kusaidia kukamatwa kwa wahusika wote wa sakata hilo na pia kuagiza uchunguzi kufanywa kwenye ofisi zote ili watakaobainika kuhusika na udanganyifu huo wafikishwe mahakamani

Waziri Lukuvi amesema zoezi hilo litakuwa endelevu nchi nzima hivyo kutahadharisha kama kuna mwekezaji yeyote aliyejipatia ardhi kwa njia ya udanganyifu bila kufuata taratibu, ni vyema akaanza upya kufuata maagizo ya serikali,na ikibainika kuna kosa popote shamba lake litafutiwa milki yake na kubadilishwa matumizi kwa mujibu wa sheria.

No comments: