TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na mabalozi wawili kutoka nchi za Qatar na Kuwait.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na mabalozi hao leo ,ofisini kwake ,Magogoni jijini Dar es salaam, Waziri Mkuu amewashukuru mabalozi hao kwa pongeza walizokuja kumpatia, pamoja na namna ambavyo nchi zao zimekua zikisaidia Tanzania, ambapo ameahidi kuendeleza ushirikiano mzuri baina ya Tanzania na nchi zao.
Kwa upande wake, Balozi wa Qatar, Abdallah Jassim al Maadad amesema Serikali yake itaendelea kuisaidia Tanzania katika maeneo yote ambayo Qatar imepiga hatua kubwa na inaweza kutoa msaada kwa Tanzania.
Amesema Quwait iko tayari kuwekeza nchini katika sekta ya kilimo, kwa vile ardhi ya Tanzania ni yenye rutuba na inafaa kwa shughuli za kilimo. Aidha, ametaja sekta nyingine ambazo wangependa kuwekeza ni pamoja na sekta ya uvuvi na viwanda.
Naye, Balozi wa Kuwait, Jasem Al Najem ambaye amekuja kujitambulisha kwa Waziri Mkuu, amesema nchi yake kupitia ‘Kuwait fund’ iko tayari kuendelea kuisaidia Tanzania katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Balozi Najem, pia ameshauri vituo vya uwekezaji vya Tanzania na Kuwait kufanya kazi kwa ushirikiano zaidi ili kurahisisha utekelezaji wa miradi mbalimbali.
(Mwisho)
Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akizungumza na balozi wa Qatar nchini, Mhe. Abdallah Jassim al Maadadi ofisini kwake jijini Dar es salaam Januari 13, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akizungumza na Balozi wa Kuwait nchini, Mhe. Jasem Al Najem, ofisini kwake jijini Dar es salaam , Januari 13, 2016. (Pichana Ofisi ya Waziri Mkuu)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P 3021,11410 DAR ES SALAAM
JUMATANO, JANUARI 13, 2016
No comments:
Post a Comment