Waziri Mkuu Atoa Ufafanuzi Kuhusu Kauli Yake Ya Kupiga Marufuku Mikutano Ya Vyama Vya Siasa - LEKULE

Breaking

28 Jan 2016

Waziri Mkuu Atoa Ufafanuzi Kuhusu Kauli Yake Ya Kupiga Marufuku Mikutano Ya Vyama Vya Siasa



Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo amefafanua kauli yake ya kupiga marufuku mikutano ya vyama vya siasa nchini  kuwashukuru wananchi hasa kwa wale wagombea walioshindwa uchaguzi  kwa kusema  kuwa mwandishi aliyeripoti tukio hilo alimnukuu vibaya.

“.......na tumesema, siasa tumeshazimaliza. Sasa tunataka tufanye kazi za maendeleo. Hatuhitaji tena watu kuja kutuvuruga. Mikutano ya shukrani itafanywa na wale tu walioshinda kwenye maeneo yao. Wengine watulie.

“Vyama sasa viache wale tu waliochaguliwa kwenye maeneo yao washukuru, wengine hawa watakuja kuleta maneno ambayo yatatuvuruga. " 
Waziri Mkuu alinukuliwa akiyasema hayo Wilayani Ruangwa mkoani Lindi

Akijibu Swali la Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani bungeni Mhe. Freeman Mbowe  leo asubuhi kuhusiana na kauli hiyo, Waziri Mkuu alisema kuwa serikali inaendeshwa kwa mujibu wa sheria na katiba hivyo inatambua kuwa katika mfumo wa vyama vingi,  vyama vya siasa vinaruhusiwa kufanya mikutano ila kwa utaratibu maalumu.

Waziri Majaliwa alisema  mwandishi aliyemnukuu kuhusiana na kauli hiyo hakumtendea haki kwa kuwa aliitoa kauli hiyo  akiwa kama mbunge wa kawaida na si Waziri mkuu na yalikuwa ni makubaliano ya vyama vya siasa katika jimbo lake  na kwamba halikuwa agizo kwa nchi nzima.

Waziri Mkuu huyo aliongeza kuwa kauli hiyo aliitoa wakati alipokutana na madiwani na viongozi wengine wa mkoa wake ambapo walikubaliana kuweka siasa pembeni na kufanya kazi kwa pamoja katika kuleta maendeleo.

No comments: