WAZIRI MBARAWA AWATAKA TEMESA KUFUNGA MITAMBO YA ELEKTRONIKI ILI KUONGEZA MAPATO - LEKULE

Breaking

14 Jan 2016

WAZIRI MBARAWA AWATAKA TEMESA KUFUNGA MITAMBO YA ELEKTRONIKI ILI KUONGEZA MAPATO

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mh.Prof. Makame Mbarawa amewataka Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA), kufunga mfumo kamili wa elekroniki katika kivuko cha Magogoni ili kudhibiti mapato yanayopotea kiholela.

Amesema takriban asilimia 20 ya abiria wanaotumia kivuko cha Mv Magogoni na Mv Kigamboni wanavuka bila kulipa nauli hali inayoathiri mapato stahiki ya kivuko hicho.

“Nawapa miezi mitatu muwe mmefunga mfumo kamili wa kupokea nauli wa elektroniki ambao utadhibiti ukwepaji wa kulipa nauli ili kuongeza mapato na kufikia shilingi milioni 25 kwa siku,” amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

Waziri Mbarawa amesema nia ya wizara yake ni kukusanya mapato stahiki kutoka katika vivuko vyote ili kuwezesha kununua kivuko vipya na kukarabati vivuko vingine kadri iwezekanavyo.

Aidha ameagia ufanyike uboreshaji wa bwalo la kupumzikia abiria upande wa magogoni ili liweze kuhudumia watu wengi na katika hali nzuri na kuagiza uboreshaji huo kuanza mara moja.

Amezungumzia umuhumi wa wafanyakazi wa vivuko vya Magogoni na kigamboni kuwa na lugha nzuri kwa abiria wao na kuwasaidia wale wenye mahitaji maaalum ili kuboresha huduma ya usafiri ya vivuko hivyo.

Ameitaka TEMESA kuweka mfumo wa tiketi za msimu zitakazowezesha wafanyakazi kulipa kwa awamu moja au mbili kwa mwaka na hivyo kunufaika na punguzo maalum na kuondoa usumbufu wa kulipa nauli kila siku.

Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa TEMESA Eng. Prisca Mkama amemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa mapato ya kivuko cha Magogoni yataimarika hivi karibuni kufuatia mikakati madhubuti wanayoifanya katika kuboresha huduma zao hususani eneo la Kigamboni.

Tariban abiria elfu 60 hutumia kivuko cha Mv. Magogoni na Mv. Kigamboni kuvuka kwa siku katika harakati za shughuli za kijamii na kibiashara.
Mkuu wa kivuko cha Magogoni Eng. Charles Irege akimwonesha Waziri wa ujenzi, uchukuzi na mawasiliano profesa Makame mbarawa namna ya kukagua tiketi za kielekroniki kabla ya abiria kuruhusiwa kuingia kwenye kivuko.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na mawasiliano profesa makame mbarawa mwenye suti akizungumza na wasafiri wa kivuko cha magogoni eneo la kigamboni kabla ya kuanza safari kulia kwake ni Kaimu mtendaji mkuu wa TEMESA Eng. Prisca Mkama.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano profesa Makame mbarawa mwenye suti akishuka kwenye kivuko cha mv. kigamboni mara baada ya kukagua shughuli za kivuko hicho.
Abiria wanaotumia kivuko cha Mv. Kigamboni wakielekea kupanda kivuko hicho kutoka magogoni kwenda Kigamboni.
Kaimu mtendaji mkuu wa wakala wa ufundi na umeme TEMESA Eng. Prisca Mkama akitoa taarifa ya utendaji wa kivuko cha Magogoni kwa Waziri wa ujenzi,uchukuzi na mawasiliano profesa Makame mbarawa kushoto na mkurugenzi wa ufundi dkt. William Nshama kulia akifuatilia.

Mkuu wa kivuko cha magogoni Eng. Charles Irege akimwonesha Waziri waziri wa ujenzi,uchukuzi na mawasiliano profesa Makame mbarawa namna ya kufuatilia mapato ya kivuko cha magogoni kwa njia ya elekroniki.

No comments: