WAZANZIBARI
leo wanasherehekea miaka 52 ya Mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964,
ambayo yaling’oa utawala wa Sultani kutoka Oman na kuwezesha wazalendo
wengi kushika hatamu ya kuongoza nchi.
Katika
kilele cha sherehe hizo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein atahutubia taifa katika uwanja wa Amaan.
Atapokea
maandamano ya wananchi wa mikoa mitano ya Unguja. Matukio mengine
makubwa yatakayofanyika katika uwanja huo ni Rais Shein kukagua gwaride
la heshima la vikosi ya ulinzi na usalama, vikiongozwa na Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) .
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na idara ya sherehe na mapambo iliyo
chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, sherehe hizo zitahudhuriwa na
viongozi wa ngazi za kitaifa akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano, John
Magufuli ambaye ni mara ya kwanza kushiriki baada ya kuchaguliwa katika
uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana.
Ratiba
hiyo inaonesha kwamba sherehe hizo, zitahudhuriwa na Makamu wa Rais,
Samia Suluhu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na marais wastaafu wa Jamhuri
ya Muungano na wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi
aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kusherehekea miaka 52 ya
Mapinduzi, yaliyowakomboa wakulima na wafanyakazi kutoka katika kucha za
wakoloni wa kisultani.
Aliwapongeza
wananchi kwa kujitokeza na kushiriki katika ufunguzi wa miradi ya
maendeleo, ambayo malengo yake ni kuharakisha maendeleo na kupambana na
umasikini.
Mitaa
mbalimbali mjini hapa, imepambwa picha za viongozi mashuhuri
waliosimama kidete kufanya Mapinduzi hayo; hususan Rais wa Kwanza, Abeid
Amaan Karume aliyeongoza timu ya watu 16 kufanya mapinduzi hayo.
No comments:
Post a Comment