SERIKALI
ipo katika hatua za mwisho za kuilipa kampuni ya Bharti Airtel ili
kurejesha umiliki wa asilimia 100 katika Kampuni ya Simu Tanzania, TTCL.
Uamuzi
huo unaotarajiwa kutekelezwa kabla ya mwisho wa mwezi huu utaiwezesha
TTCL kurejesha hisa zake 35% zilizonunuliwa na Airel mwaka 2001 na
kuifanya Bharti Airtel kuwa mbia mwenza katika Kampuni hiyo.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof Makame Mbarawa ametangaza
uamuzi huo Jumatatu hii Mkoani Mtwara alipotembelea Ofisi za TTCL Mkoa
wa Mtwara, kukagua mitambo na miundo mbinu ya Mkongo wa Taifa wa
Mawasiliano.
"Serikali
imesikia kilio cha muda mrefu cha Watanzania na wadau wote wa TTCL
kuhusu kuondoka kwa mbia mwenza Kampuni ya Bharti Airtel. Ubia huu wa
TTCL na Bharti Airtel utahitimishwa Rasmi kabla ya mwisho wa mwezi huu.
"Tumefanya
majadiliano ya kutosha, tumekubaliana kuwa Serikali iilipe Bharti
Airtel sh bilioni 14.9 ili kurejesha hisa za 35% za TTCL na kuifanya
Kampuni hii ya TTCL kuwa mali ya Umma kwa 100%.
"Tutatumia
fedha za Mapato ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kukamilisha
utaratibu huu. Naiagiza Bodi na Menejimenti ya TTCL kufanya kazi kwa
bidii na Ufanisi Mkubwa na kusimamia kikamilifu shughuki za TTCL ili
kutimiza jukumu lake kwa Umma." Alisema Waziri Mbarawa
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Prof. Tolly Mbwette amesema,
kukamilika kwa mchakato huu ni hatua muhimu sana kwa Uhai na ufanisi wa
TTCL na kusisitiza kuwa, mpango wa mageuzi ya kibiashara wa kampuni hiyo
sasa utatekelezeka kwa kasi kubwa baada ya hatua hii.
Ofisa
Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk. Kamugisha Kazaura amesema, jitihada kubwa za
TTCL sasa zitaelekezwa katika kuboresha huduma kwa kutumia fedha za
ndani na Mikopo ya wadau wa kibiashara ili kuiwezesha kampuni kuendelea
kuwa kiongozi katika utoaji wa huduma bora na nafuu katika soko la
Mawasiliano nchini.
Hivi karibuni, TTCL imezindua huduma za Mtandao wenye kasi zaidi wa 4G LTE na kuimarisha ubora wa huduma zake za data na sauti.
Aidha,
TTCL na Benki ya TIB zimeingia makubaliano ya mkopo wa fedha na dhamana
za Benki utakaoiwezesha TTCL kupata fedha dola za Marekali milioni 329
ili kuingiza mitambo mipya ya kisasa itakayo boresha huduma zake ikiwa
ni pamoja na kuanzisha huduma ya miamala ya fedha kwa njia ya mtandao.
No comments:
Post a Comment