Tanesco Yazuia Shughuli za Kilimo Karibu na Nguzo - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Wednesday, 20 January 2016

Tanesco Yazuia Shughuli za Kilimo Karibu na NguzoSHIRIKA la Umeme (Tanesco) limetoa angalizo kwa wanaoendesha shughuli za kilimo, kwa kuwaambia hawatakiwi kulima karibu na nguzo kwani wanapaswa kuacha meta 30 kila upande.

Meneja wa Tanesco wa Mkoa wa Shinyanga, Mathias Solongo alitoa angalizo hilo kutokana na kuwapo malalamiko ya wananchi zaidi ya 50 wa kijiji cha Seseko kata ya Mwamalili manispaa ya Shinyanga, dhidi ya Tanesco kuwakatia mazao.

Alisema wananchi hawaruhusiwi kulima sehemu zilizo karibu na nguzo za umeme ikizingatiwa kwamba, walishalipwa na manispaa hakuna sehemu ambayo haijalipwa.

“Na inayotakiwa kulipa ni manispaa siyo shirika na tayari ilishawalipa na katika nguzo hizo wananchi kweli hawatakiwi kulima, wanatakiwa kuacha mita 30 kila upande lakini tofauti ya hapo haitakiwi,” alisema.

Akizungumzia wananchi hao wanaolalamikia shirika, Solongo alishauri viongozi wa wananchi waende kwake azungumze na kuwaelewesha vizuri suala hilo.

Awali, wakizungumza na waandishi wa habari, wananchi hao wa kijiji cha Seseko, kata ya Mwamalili walisema miaka yote walikuwa wakiendelea kulima na hawakuwa na taarifa ya kuwakataza.

“Sisi tunachohitaji ni kulipwa mazao yetu yaliyokatwakatwa ambayo yamekatwa kimakosa kwani hata yakiiva hayafiki kwenye nguzo za umeme, baada ya hapo tulipwe fidia yetu ya ardhi kwani bado hatujalipwa. 

“Wamekata mtama wangu na mahindi yangu nitakula nini na watoto wangu, halafu wamekata bila hata kunitaarifu,” alisema William Deus.
Post a Comment