Waziri
wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo ameanza ziara yake Mkoa wa
Njombe kwa kutembelea Mradi wa Kufua Umeme kwa kutumia mabaki ya miti ya
Miwati (TANWAT.)
Baada
ya kukagua mradi huo, Prof Muhongo ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) kufanya majadiliano na TANWAT ili waongeze uzalishaji kutoka
Megawati 2.5 za umeme hadi kufikia Megawati 10.
Aidha,
ameagiza TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini REA kufanya majadiliano
na TANWAT ili kuanza kununua nguzo zinazozalishwa na kampuni hiyo yenye
uwezo wa kuzalisha nguzo 120,000 kwa mwaka badala ya kununua nguzo hizo
katika nchi za Kenya, Zambia, Uganda na Afrika Kusini.
"REA
na TANESCO watakuja hapa kuangalia hizi nguzo na kufanya ukaguzi kama
zinakidhi viwango vya TANESCO. Ikiwa zinakidhi viwango REA wawaelekeze
Wakandarasi kununua nguzo za TANWAT kwa kufuata taratibu za manunuzi," ameongeza Prof. Muhongo.
Pia
Prof. Muhongo amewataka TANESCO kubadilika kiutendaji na kuongeza wigo
wa uzalishaji umeme kwa kuwatumia wazalishaji wakubwa, wa kati na wadogo
ambao wote kwa pamoja watasaidia kuondoa tatizo la uhaba wa nishati
hiyo.
Akikagua
Mradi wa kufua umeme wa Uwemba, Prof Muhongo ameiagiza TANESCO Njombe
kuandaa orodha ya vyanzo vya umeme vinavyotokana na maji vilivyo katika
gridi na visivyo katika gridi na kujadiliana na wazalishaji ili
kukubaliana nao kuuziana umeme
"Uzalishaji
umeme kutumia maji ndio rahisi zaidi. TANESCO angalieni orodha hiyo,
wawaeleze Mikataba yao muone namna ya kuuziana umeme. Bila umeme huwezi
kuzalisha ajira na bila umeme wa uhakika hatuwezi kuwa na viwanda vya
kutosha," alisema.
Waziri
Muhongo ameongeza kuwa ni wajibu wa Serikali kuwasaidia na kufanya kazi
na wazalishaji wadogo wa umeme ili waweze kuongeza kiwango cha
uzalishaji umeme hivyo pia ameutaka Mkoa wa Njombe kufuatilia kwa pamoja
na TANESCO suala hilo na kulifanyia kazi.
Vilevile,
aliwataka TANESCO kukaa na wazalishaji wadogo ili kuangalia bei zao,
jambo ambalo litaiwezesha Serikali kujua bei kwa lengo la kuhakikisha
kwamba bei hizo hazimuumizi mwananchi.
Aidha,
Profesa Muhongo aliwaagiza TANESCO kufanya ukarabati wa mashine
zilizoharibika ili ziendelee kufanya kazi kwa ajili ya kuongeza
uzalishaji.
Kwa
upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Jackson Saitab aliahidi
kuyafanyia kazi maagizo yote ya Waziri na kuongeza kuwa, nishati ni
sekta muhimu hata katika uongezaji thamani ya mazao.
No comments:
Post a Comment