Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Charles Kitwanga amesema zoezi linaloendelea sasa la kukamata raia wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi hapa nchini bila vibali halitawagusa wageni wenye vibali halali.
Mheshimiwa Kitwanga ameyasema haya mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na jumuiya ya raia toka nchini China wakati wa sherehe zilizoandaliwa na raia hao katika Hoteli ya Golden Tulip jijini Dar es Salaam.
Katika sherehe hizo ambazo ziliandaliwa mahsusi kuukaribisha mwaka Mpya wa Kichina, Mheshimiwa Kitwanga alisema uhusiano wa Tanzania na China ulianzishwa na marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Kiongozi wa China, marehemu Mao Zedong zaidi ya miaka hamsini iliyopita.
Amesema uhusiano huo umeendelea kuimarishwa hadi katika nyanja za kiuchumi ambapo hadi sasa kuna zaidi ya Kampuni 500 za Kichina ambazo zinafanya shughuli za kibiashara hapa nchini ambazo zimetoa zaidi ya nafasi 100,000 za kazi kwa Watanzania.
Mheshimiwa Kitwanga alitumia fursa ya sherehe hizo kuwahakikishia wawekezaji wote waliopo hapa nchini kuwa Serikali ya Tanzania italinda biashara zao kufuatana na sheria za nchi.
Kuhusu zoezi linaloendelea hapa nchini la kukamata wageni ambao wanaishi na kufanya kazi bila vibali halali alisema kumekuwa na taarifa za uzushi zinazoenezwa hapa nchini na nje ya nchi kuwa Serikali ya Tanzania inawafukuza wageni kwa vile haihitaji raia wa kigeni hapa nchini.
Amesema taarifa hizo ni za uongo zinazolenga kuichafua Tanzania katika jumuiya ya kimataifa na kusema raia wa kigeni wanaokamatwa ni wale tu wasio na vibali halali vya kuishi na kufanya kazi hapa nchini.
Amesema zoezi hilo ni la kawaida na linafanywa kufuatana na Sheria za Uhamiaji lakini halitawahusu wageni wenye vibali halali vya kufanya kazi na kuishi nchini.
Kati ya mwaka 2014 na Januari 2016 Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imetoa vibali vya ukaazi kwa jumla ya wageni 40,765 toka mataifa mbalimbali na idadi hiyo inaendelea kuongezeka siku hadi siku.
Wageni waliofukuzwa kwa sababu mbalimbali mwaka 2015 ni 1,642.
Aidha, kati ya 08 Desemba, 2015 na 14 Januari, 2016 raia wa kigeni waliokamatwa kwa kuishi na kufanya kazi nchini bila vibali halali ni kama ifuatavyo:
- Burundi 284
- Kenya 26
- Uganda 13
- Somalia 7
- Ethiopia 157
- DRC 34
- China 285
- India 41
- Zambia 40
- Nigeria 08
- Lebanon 01
- Ivory Coast 10
- Madagascar 05
- Malawi 27
- Korea 09
- Zimbabwe 01
- Ghana 01
- Rwanda 03
- Afrika Kusini 01
- Wenye uraia wa utata 11.
Kati ya hawa, wengine wamemepelekwa katika kambi za wakimbizi, hasa raia waliotokea Burundi, wengine wamepewa amri ya kuondoka nchini na wengine kesi zao ziko katika hatua mbalimbali mahakamani.
MWISHO
MWISHO
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi – 24 Januari, 2016
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi – 24 Januari, 2016
No comments:
Post a Comment