Spika wa Bunge Kutangaza Kamati Za Bunge Leo - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Monday, 11 January 2016

Spika wa Bunge Kutangaza Kamati Za Bunge Leo


Spika wa Bunge, Job Ndugai, anatarajia kutangaza kamati za Bunge leo chini ya utaratibu mpya na kwamba leo atatangaza Kamati ya Kanuni pekee.

Baada ya kuitangaza kamati hiyo, nyingine zilizobaki atazitangazia mjini Dodoma wakati vikao vya Bunge vitakapokuwa vikiendelea mwishoni mwa mwezi huu.

Utaratibu huo umebainishwa na Ndugai jana alipoulizwa  iwapo Kamati za Bunge zitatangazwa kabla ya kuanza kwa Bunge lijalo Januari 26, Mwaka huu.

“Kesho (Leo) nitatangaza kamati moja tu ya kanuni na nyingine nitazitangazia mjini Dodoma kabla ya kuanza kwa Bunge lijalo,” alijibu kwa ufupi.

Taarifa za kuaminika zinasema kwamba Spika Ndugai amepanga kupunguza wingi wa Kamati za Bunge ili kuendana na uchache wa wizara zilizopo.

Taarifa zaidi zinasema kuwa sababu kubwa ya kufanya hivyo ni kuhakikisha kamati zinakuwa chache lakini zilizo na uwezo wa kufanyakazi kwa kasi ambayo itaisaidia serikali ya awamu ya tano.

Baada ya leo kutangaza Kamati ya Kanuni, Spika Ndugai atabaki na jukumu la kutangaza kamati nyingine 14 mjini Dodoma, iwapo hakutakuwa na ongezeko la kamati.

Kamati za Bunge huundwa kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 96, likiwa limepewa madaraka ya kuunda kamati za Bunge za aina mbalimbali na muundo wake umefafanuliwa na Kanuni za Kudumu za Bunge.

Katika muundo huo zipo kamati za kisekta na zile zisizokuwa za kisekta, ambazo kwa pamoja hufanyakazi na kutekeleza majukumu yao kwa niaba ya Bunge.


Kwa mujibu wa Kanuni ya 89 Bunge limeunda Kamati 15, ambapo baadhi ya kamati hizo ni Kamati ya Haki, Maadili, Kinga na Madaraka ya Bunge na Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara.
Post a Comment