RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
ametoa risala ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2016 kwa wananchi na kueleza
kuwa takwimu za mwanzo wa mwaka 2015, uchumi wa Zanzibar umeendelea
kuimarika.
Katika
risala yake hiyo kwa wananchi, Dk. Shein alisema kuwa huduma za jamii
zikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama, huduma za afya pamoja na
elimu nazo zimeimarika ikiwa ni pamoja na kupiga hatua kubwa katika
kuimarisha miundombinu.
Dk.
Shein alisema kuwa ujenzi wa barabara muhimu umemalizika na kuzinduliwa
Unguja na Pemba pamoja na kukiimarisha kiwanja cha ndege cha Kimataifa
cha Abeid Amani Karume, pamoja na Kiwanja cha ndege cha Pemba ambacho
tayari kimeshatiwa taa za kurukia ndege.
Alisema
kuwa hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa viwanja hivyo tayari imepelekea
kuwepo kwa ongezeko kubwa la idadi ya ndege za Kimataifa zinazokuja
Zanzibar, jambo ambalo limepelekea kuimariska kwa sekta ya Utalii na
shughuli za biashara.
Dk.
Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba
imefanikiwa kutengenezesha meli mpya yenye mitambo ya kisasa katika
Kampuni ya ‘Daewoo International’ ya Jamhuri ya Korea, ambayo ina
utaalamu na uzoefu mkubwa wa kutengeneza meli.
“Nasaha
zangu kwenu nyote wananchi ni kuwa tuithamini na kuienzi meli yetu
hiyo... tukumbuke msemo wa Marehemu Mzee Abeid Amani Karume kuwa
‘kithamini chako mpaka usahau cha mwenzako”, alisema Dk. Shein.
Aidha,
Dk. Shein katika risala hiyo alieleza kuwa katika mwaka 2015 Serikali
imefanya juhudi kubwa katika kuhakikisha dhamira ya kujenga bandari ya
Mpiga Duri inaanza kutekelezwa, ambapo ujenzi huo unatarajiwa kuanza
wakati wowote katika mwaka 2016.
Dk.
Shein alieleza juhudi zilizochukuliwa katika kusambaza umeme vijijini
Unguja na Pemba ikiwa ni pamoja na kuufikisha umeme huko Kisiwa Panza na
Kisiwa cha Makoongwe kwa upande wa Pemba, kwa kuwatumia wataalamu
wazalendo.
Kwa
upande wa huduma za afya Dk. Shein alisema kuwa katika mwka 2015 huduma
hizo zimeimarishwa kwa kuongeza kasi ya kusomesha wataalamu,
upatikanaji dawa na huduma mbali mbali pamoja na kuziimarisha hospitali
kwa kutekeleza miradi ya ujenzi.
Akieleza
kuhusu kuimariaka kwa sekta ya elimu mnamo mwaka 2015, Dk. Shein
alisema kuwa mafanikio makubwa yamepatikana ikiwa ni pamoja na kuanza na
kumalizika kwa miradi ya ujenzi wa skuli, kuongeza fani za mafunzo
katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu sambamba na kutekeleza
lengo la kuondoa gharama za kuchangia elimu mashuleni.
“Lengo
letu ni kuifanya elimu ya msingi kuwa bure huku tukiandaa utaratibu ili
elimu ya sekondari nayo iwe bure kama ilivyodhamiriwa na Muasisi wa
Mapinduzi yetu ya mwaka 1964”,alisema Dk. Shein.
Alieleza
kuimarika kwa miradi ya ujenzi wa miji na majengo ya kisasa katika
sehemu mbali mbali ili kuweza kuijenga taswira mpya ya Zanzibar katika
kipindi kifupi kijacho. Aidha, alieleza kukamilika kwa viwanja vya
kufurahishia watoto hapa nchini.
Aidha,
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi wote kuwa walinzi
wa miundombinu iliyopo na wasichelee kuwafichua wale wote wanayoiharibu
na kueleza kusikitishwa kwake katika mwaka uliomalizika baadhi ya watu
waliiharibu miundombinu hiyo kwa kuweka mbele maslahi yao binafsi na
kusahau maslahi ya wote.
Sambamba
na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa Serikali inaendelea kutoa ruzuku kwa
huduma za matrekta na pembejeo za kilimo kwa wakulima ambao kwa msimu wa
mwaka 2015/2016 tani 750 za mbolea na lita 15,000 za dawa ya kuulia
magugu zimekwishanunuliwa.
Kwa
upande wa zao la Karafuu Dk. Shein alisema kuwa wakulima wameitikia
vyema wito wa Serikali wa kuuza karafuu zao katika vituo vya ZSTC,
ambapo katika msimu wa ununuzi wa karafuu wa mwaka 2015/2016, hadi
kufikia mwezi Novemba, 2015 jumla ya tani 962.7 za karafuu zenye thamani
ya Tshs. Bilioni 13.471 zimenunuliwa katika vituo vya ununuzi wa
karafuu vya SSTC Unguja na Pemba.
Akieleza
kuhusu uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 25, Oktoba mwaka 2015 ambapo
wananchi wa Zanzibar walishiriki katika kuwachagua viongozi wao, ambapo
kwa upande wa uchaguzi wa viongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
uliosimamiwa na Tume ya Taifa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
umemaliza na CCM kupata ushindi, Dk. Shein alitumia fursa hiyo
kumpongeza Mhe. Dk. John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa
kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais.
Aidha,
Dk. Shein alieleza kuwa kwa upande wa Zanzibar Tume ya uchaguzi
uliufuta uchaguzi huo tarehe 28 Oktoba, 2015 baada ya kubainika kutokea
kwa kasoro kadhaa kama zilivyoelezwa na Tume hiyo.
Dk.
Shein alisema kuwa katika suala zima la hali ya kisiasa ya Zanzibar,
iliyojitokeza baada ya kufutwa kwa uchaguzi mkuu, viongozi walishauriana
kukutana ili kufanya mazungumzo ya kutafuta suluhu kwa njia ya amani,
ili nchi iendelee kuwa na amani, umoja na mshikamano na hatimae
wakakubaliana kuanza mazunguzmo hayo.
Kwa
mujibu wa maelezo ya Dk. Shein katika risala hiyo, mazungumzo hayo
yanayowahusisha viongozi sita yamefikia hatua kubwa na bado yanaendelea
na kueleza kuwa taarifa kamili ya mazungumzo hayo itatolewa mara
yatakapokamilika.
Pamoja
na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi kuwa tarehe
12 Jamuari 2016 Zanzibar itaadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi ambapo kama
kawaida, sherehe hizo zitatanguliwa na matukio mbali mbali ya shughuli
za uzinduzi wa miradi ya maendeleo na uwekaji wa mawe ya msingi.
Dk.
Shein alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa
wingi katika matukio mbali mbali yaliopangwa katika maadhimisho hayo
ambapo pia, kushiriki kwao kwenye sherehe ya maadhimisho hayo ni hatua
ya kuyaendeleza malengo ya Mapinduzi kwa shabaha ile ile waliokuwa nayo
waasisi wa Zanzibar.
Dk.
Shein pia, alitoa wito kwa wananchi kuzingatia kanuni za afya kwa
kuimarisha usafi na kuzitaka Baraza la Manispaa na Mabaraza ya Miji kwa
Pemba na Halmashauri zote za Wilaya kuchukua hatua za uzoaji wa taka, na
kuwataka wananchi wote kushiriki katika kuisafisha miji na maeneo
wanayoishi hapo siku ya Januari 3 mwaka 2016.
Sambamba
na hayo, Dk. Shein aliwakumbusha wananchi kuwa tarehe 1 Januari ni siku
ya kujitokeza kufanya mazoezi hivyo wajitokeze kwa wingi kufanya
mazoezi.
No comments:
Post a Comment