Wataalam kutoka Shirika la Umeme (Tanesco) pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), wanaendelea kupiga hesabu kabla ya kuja na majawabu ya kushusha bei ya umeme.
Aidha, Profesa Muhongo alisema, kwa mara ya kwanza, wanataka nyaya zote za umeme jijini Dar es Salaam hususan katikati ya jiji, zipite chini ya ardhi.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema jana bungeni kwamba bei hiyo itashuka kwa mchakato huo (wa kupiga hesabu) na si kwenye majukwaa.
Alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) aliyetaka kufahamu hatua ambazo serikali imefikia katika uzalishaji, usambazaji na umeme kwa ubia.
“Kuhusu bei ya umeme, wengine wanasema nilisema ishuke haijashuka…nilisema tunapiga hesabu. Bei huwezi kuongea kwenye majukwaa. Tanesco na Ewura wanapiga hesabu tunataka kushusha bei na si kwenye majukwaa,” alisema.
Kwa upande wa nyaya za umeme, alisema mkandarasi ameelekezwa ifikapo Aprili mwaka huu, serikali iachane na kesi za nyaya kuanguka kwa kuwa zitakuwa zimepitishwa chini ya ardhi.
“Kwa mara ya kwanza, Serikali inataka nyaya zote za umeme zipite chini ya ardhi,” alisema na kufahamisha bunge kwamba, maeneo ya Mbagala na Temeke, inajengwa transfoma kubwa.
Pia kwa upande wa Jimbo la Kibamba, inaondolewa transfoma yenye kilovolti 100 a kuwa na yenye kilovolti 2000.
Alisema Tanzania ijayo itakuwa ya umeme mwingi na wa bei nafuu ambapo inatarajia kuwa na umeme wa megawati 10,000. Profesa Muhongo alisema serikali inaendelea kukaribisha wawekezaji na kwamba Tanzania ijayo itakuwa ya umeme mwingi na wa bei nafuu.
Akizungumzia suala la usambazaji umeme, alisema kuna miradi kadhaa inaendelea kutekelezwa na serikali kwenye maeneo mbalimbali nchini. Profesa Muhongo alisema umeme uliopo hivi sasa hauvuki megawati 1,500 na ili kufikia lengo wanahitaji kufikia megawati 10,000.
Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (CHADEMA), Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani, alisema ukarabati wa miundombinu katika jimbo hilo, unatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia mwanzoni mwa mwezi ujao na kukamilika Juni, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment