CCM
imemjibu mwanasheria Mkuu wa Chadema ikisema ili chama hicho kikuu cha
upinzani kionekane kinapambana na ufisadi kwa vitendo, kinatakiwa
kumuunga mkono Rais John Magufuli na kumvua uanachama Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, katibu wa itikadi na
uenezi wa chama hicho tawala, Nape Nnauye alisema Chadema iliachana na
ajenda ya kupambana na ufisadi baada ya kumpokea Lowassa Julai mwaka
jana baada ya jina lake kukatwa katika mchakato wa CCM kusaka mgombea
wake wa urais.
“Sisi
hatukumpitisha (Lowassa) awe mgombea wetu wa urais kwa sababu hiyo (ya
ufisadi) na ndiyo maana yeye mwenyewe aliamua kuondoka na kwenda
Chadema,” alisema Nape.
“Hata katika kampeni za uchaguzi mkuu, Chadema hawakuzungumzia ajenda ya ufisadi, ni kama Lowassa aliifunika tu.”
Alikuwa
akimjibu Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu ambaye juzi alisema
ufisadi ni ajenda ya kudumu ya chama hicho kwa kuwa Rais Magufuli
hataweza kuufumua wote katika kipindi cha miaka mitano.
Huku
akichelea kueleza kiundani sababu za CCM kutomfukuza Lowassa kwa tuhuma
za ufisadi mpaka alipoamua kujiondoa na kujiunga na Chadema, alisema
kauli ya Lissu inalenga kuwahadaa Watanzania.
“Kauli
ya Lissu ni ya kushangaza sana. Sisi tunajua jinsi ambavyo Chadema na
washirika wake walivyojitenga na ajenda ya ufisadi. Kama kweli
wanaupinga, basi wamuunge mkono Rais Magufuli ambaye kwa sasa anapambana
na ufisadi kwa kasi,” alisema mbunge huyo wa Mchinga.
“Wakati
mwingine kila jambo hufanyika kwa wakati wake. Suala la kupinga ufisadi
CCM lilianza siku nyingi tangu enzi za kujivua gamba. Tumeendelea nalo
mpaka watu wakajiondoa wenyewe,” alisema Nape.
Alisema
hoja ya kupinga ufisadi ndani ya CCM ilikibeba chama hicho katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na kikapata ushindi mnono, huku Chadema
iliyokuwa ikilia na ufisadi ikishindwa.
“CCM tulieleza sababu za kutompitisha Lowassa kugombea urais na hilo lilikuwa wazi,” alisema.
Katika
ufafanuzi wake wa juzi, Lissu alisema ili apambane na ufisadi, Rais
Magufuli anapaswa kuacha tabia za CCM na kumtaka mwenyekiti wa Tume ya
Uchaguzi Zanzibar (ZEC) amtangaze mshindi halali wa Uchaguzi Mkuu ambao
Chadema wanaamini Maalim Seif Sharif Hamad alishinda.
Pia
Lissu alimtaka Rais ataje majina ya waliokwepa kodi ili kama
watajitokeza kuwania uongozi, wadhibitiwe kwa kuwa Katiba imezungumza
kwa maneno makali dhidi ya vitendo hivyo viovu.
Aidha,
aliponda uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo anayetajwa kuhusiska katika sakata la uchotwaji wa Sh3060
bilioni kutoka akaunti ya Tetega Escrow.
Miaka 39 ya CCM
Akizungumzia
maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 39 ya kuzaliwa kwa CCM, Nnauye
alisema uzinduzi utafanyika Januari 31, visiwani Zanzibar na mgeni rasmi
atakuwa makamu mwenyekiti wa chama hicho na Rais wa Zanzibar, Dk Ali
Mohammed Shein.
Alisema
kilele cha maadhimisho hayo kitakuwa Februari 6, mjini Singida na
yataongozwa na mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete ambaye aliiongoza
Serikali ya Awamu ya Nne.
“Viongozi
wa kitaifa na baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu watakaohudhuria
maadhimisho haya watapangiwa shughuli za ujenzi wa chama na taifa katika
wilaya zote za mkoa wa Singida, siku tatu kabla ya kilele cha
maadhimisho,” alisema.
Alisema
mikoa yote nchini inapaswa kuandaa shughuli hiyo wiki moja kabla ya
maadhimisho, na kwamba lengo ni kufanya shughuli za ujenzi wa chama
hicho katika maeneo yao.
“Tutakachokifanya
wiki hiyo ni kupokea wanachama wapya, kufanya mikutano ya kuwashukuru
wananchi kwa kuiamini CCM na kuichagua iendelee kuongoza, kuhamasisha
wananchi kufanya kazi ili kujiletea maendeleo,” alisema.
No comments:
Post a Comment