Naibu Waziri wa Ajira Afuta Kibali cha Kazi cha Raia Wa Kigeni....... Aviadhibu Viwanda vya Lodhia na Sunflag kwa Kukiuka Taratibu za Kazi - LEKULE

Breaking

6 Jan 2016

Naibu Waziri wa Ajira Afuta Kibali cha Kazi cha Raia Wa Kigeni....... Aviadhibu Viwanda vya Lodhia na Sunflag kwa Kukiuka Taratibu za Kazi


NAIBU Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde amevitoza faini ya zaidi ya Sh milioni 60 viwanda viwili vya Lodhia Plastic Industries Limited na Sunflag (T) Ltd kwa kukiuka taratibu za kazi na kudharau mamlaka ya usalama mahali pa kazi (Osha).

Mavunde alitoa adhabu hiyo jana jijini hapa wakati alipofanya ziara ya kushtukiza kwenye viwanda hivyo huku akiongozana na wakuu wa idara ya kazi, idara ya uhamiaji na viongozi kutoka Osha.

Awali alipokuwa katika kiwanda cha Sunflag, alizungumza na baadhi ya wafanyakazi na kugundua kuwa baadhi yao hawana mikataba ya ajira na wamefanya kazi zaidi ya mwaka mmoja lakini pia hawana vifaa vya kutosha vya kuzuia pamba kuingia mwilini.

Pia aliagiza menejimenti ya kiwanda hicho, kuhakikisha inalipa mishahara ya wafanyakazi kwa kima cha Serikali na si kuwalipa Sh 4,424 kwa siku. Aidha akiwa kiwandani hapo aligundua kuwa kuna wafanyakazi raia wa kigeni 41 wanaofanya kazi katika idara mbalimbali zinazopaswa kusimamiwa na raia wa Tanzania.

Akiwa katika kiwanda cha Lodhia, Mavunde alifuta kibali cha mmoja wa wageni kutoka nje ya nchi kutokana na kukiuka kibali cha kufanyakazi na kumwagiza Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Raju Sighn kupeleka vibali 38 vya raia wa kigeni ili vikaguliwe.

Kutokana na kasoro hizo Mavunde alitoza faini ya jumla ya Sh milioni 22.9 kwa kiwanda cha Sunflag na kiwanda cha Lodhia Plastic kilitozwa Sh milioni 10 kutokana na kukiuka masharti ya uendeshaji viwanda na kutoa siku 14 faini hiyo iwe imelipwa.


“Ndani ya siku saba muwe mmepeleka taarifa Osha na hivi vibali vya wageni kutoka nje ya nchi kwa ofisi za kazi jijini Arusha. Maana mnasema mna vibali lakini nilivyoviona havijaniridhisha, pelekeni ili waone na ikithibitika mmekidhi viwango mtapunguziwa adhabu, ila heshimuni sheria za nchi,” alisisitiza.

No comments: