Operesheni
kubwa ya kubomoa nyumba zaidi ya 15,000 zilizojengwa katika maeneo
yasiyostahili jijini Dar es Salaam, imekumbana na changamoto ya aina
yake baada ya mmoja wa wasimamizi wa kazi hiyo kutoka Baraza la Taifa la
Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (Nemc), Heche Suguti, kuanguka
ghafla akiwa ofisini kwake na kuwahishwa hospitali akiwa hoi.
Chanzo
kutoka ndani ya Nemc kimesema kuwa Suguti ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha
Sheria katika baraza hilo, alianguka ofisini kwake majira ya saa 9:30
alasiri baada ya kurejea kutoka katika Mahakama Kuu kitengo cha ardhi
kushughulikia kesi inayoikabili Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi dhidi ya wakazi 681 wa eneo la Mkwajuni, Kinondoni ambao
wanapinga nyumba zao kubomolewa.
Taarifa
zaidi zinaeleza kuwa baada ya Suguti kuanguka ghafla ofisini kwake eneo
la Mikocheni, baadhi ya wafanyakazi wenzake (wa Nemc) walimsaidia
haraka kwa kumbeba na kumpakiza kwenye gari na kumpeleka hospitali mbili
tofauti ambako kote vipimo vya awali havikubaini tatizo.
“Baadaye
alipelekwa katika Hospitali ya Aga Khan ambako alilazwa kuanzia siku
hiyo (Jumanne) na kutolewa leo asubuhi (jana) baada ya kupata nafuu… ila
kwa kifupi ni kwamba afya yake imeyumba na hadi sasa madaktari bado
wanachunguza kujua ni kitu gani hasa kinachomsumbua,” chanzo kiliiambia Nipashe jana.
Mkurugenzi
wa Nemc, Bonaventure Baya, alikiri kuwa Suguti aliugua baada ya
kuanguka ofisini Jumanne wiki hii na kulazwa katika Hospitali ya Aga
Khan, lakini haoni kama ni sahihi kuzungumzia afya yake kwani hayo ni
masuala binafsi.
“Nadhani ni uchovu ndiyo uliokuwa unamsumbua… hata hivyo, hayo ni masuala binafsi. "
Alipotafutwa
kwa njia ya simu jana mchana, Suguti aliyekuwa akizungumza kwa taabu,
alikiri kupatwa na tatizo asilolifahamu na kuanguka ofisini kabla ya
kujikuta akiwa amelazwa katika wodi mojawapo ya Hospitali ya Aga Khan.
“Kwakweli
sielewi kilichotokea. Nilipoingia ofisini kwangu baada ya kutoka kwenye
kesi ya nyumba za watu wa Kinondoni, ghafla nikahisi kizunguzungu, giza
kutanda na mwishowe nikaanguka… sijui kilichotokea baada ya hapo ila
fahamu ziliponirudia nikajikuta nikiwa hospitali,” alisema Suguti.
Alipotakiwa kueleza zaidi kuhusiana na tukio hilo, Suguti hakuwa tayari kwa maelezo kuwa bado hajisikii vizuri.
“Kwa sasa naomba uniache tu, sijisikii kuzungumza zaidi,” alisema na kukata simu.
Zaidi
ya nyumba 16,000 zimeshawekwa alama ya X katika maeneo mbalimbali ya
jiji la Dar es Salaam ambazo zinatakiwa kubomolewa kutokana na kujengwa
maeneo hatarishi.
No comments:
Post a Comment