Mwanamke
mmoja (jina linahifadhiwa) anayedaiwa ni mke wa mtu, amefariki dunia
katika nyumba ya kulala wageni katika Manispaa ya Bukoba, akiwa na
mwanaume mwingine anayesemekana ni hawara yake.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi, amethibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kueleza kuwa, watu hao walienda katika nyumba hiyo ya
kulala wageni iliyopo eneo la Hamugembe Januari 3, mwaka huu na kuchukua
chumba namba nane.
Alisema
siku iliyofuata saa 6:00 mchana, polisi walipokea taarifa kutoka kwa
wahudumu wa nyumba hiyo ya kulala wageni kuwa katika chumba hicho kuna
watu waliingia jana yake lakini hadi muda huo mlango wa chumba ulikuwa
haujafunguliwa na kuna ukimya uliowatia hofu.
Alisema
wahudumu hao waliambatana na polisi na walipofika eneo la nyumba hiyo
walimkuta mmiliki wake ambaye alitoa funguo za akiba na kufungua chumba
hicho.
“Polisi
walipofungua chumba walikuta godoro liko chini lakini kitandani
lilipopaswa kuwa kulikuwa na mwili wa mwanamke ukiwa umefunikwa shuka na
kuuchukua kwenda kuuhifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Kagera,” alisema.
Kamanda
huyo wa polisi mkoa wa Kagera, alisema mtu aliyekuwa pamoja na mwanamke
huyo (jina linahifadhiwa) ambaye ni dereva wa basi la abiria
linalofanya safari zake kati ya Bukoba na Mwanza, hakukutwa katika
chumba hicho na alifunga mlango kwa nje na kuondoka na funguo.
Hata
hiyo, alisema chanzo cha kifo hicho hakijajulikana lakini kutokana na
taarifa walizopata kutoka kwa msaidizi wa dereva huyo wamefanikiwa
kumpata mtu aliyejitambulisha kuwa ni mume wa marehemu.
Kamanda
Ollomi aliongeza kusema kuwa, mume wa marehemu mkazi wa Butimba,
jijini Mwanza, amepatikana na kukabidhiwa mwili wa mkewe, huku uchunguzi
wa tukio hilo ukiendelea na kwamba wafanyakazi wawili wa nyumba hiyo ya
kulala wageni wanashikiliwa na polisi kwa upelelezi zaidi lakini pia
kwa kitendo cha kuficha taarifa za wageni wanaolala katika nyumba hiyo.
No comments:
Post a Comment