Medeye na Guninita Wamvaa Benard Membe Baada ya Kusema Hujisikia Kichefuchefu Akionana na Makada Walioihama CCM - LEKULE

Breaking

24 Jan 2016

Medeye na Guninita Wamvaa Benard Membe Baada ya Kusema Hujisikia Kichefuchefu Akionana na Makada Walioihama CCM


Siku moja baada ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kusema akionana na waliokuwa wanachama wa CCM na kuhamia upinzani anajisikia kichefuchefu, waliokuwa makada wa chama hicho wamemshukia kwa kauli yake hiyo.

Membe alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akitoa maoni yake kuhusu makada waliohama na kusisitiza kuwa wasipokewe endapo watataka kurudi.

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole Medeye ambaye alitimkia Chadema, alisema kama angesikia maneno hayo kwa mtu mwingine asingeshangaa, lakini siyo kwa Membe.

Mbunge huyo wa zamani wa Arumeru – Magharibi, alisema Membe anapata masilahi yake kwa kutambulika kama waziri mstaafu na wakati anaapa kuwa katika nafasi hiyo alitumia Katiba ambayo hivi sasa kwa kupinga yaliyomo ikiwamo uhuru wa mtu kujiunga na chama chochote cha siasa, anakosea.

Medeye alisema kwa kauli hiyo, Membe hana haki ya kugombea nafasi yoyote ya siasa kwa sababu haamini katika vyama vingi wakati Taifa linaendeshwa kwa Katiba inayokubali suala hilo.

Alisema hata kauli ya Membe ya kutounga mkono uchaguzi kurudiwa Zanzibar akitaka kufanyiwa kazi kasoro chache ni ya kinafiki kwa sababu ameonyesha kutopenda upinzani.

“Hana msimamo hazungumzi vitu kutoka moyoni, kama kweli anakubali vyama vingi na ana uchungu na kinachoendelea Zanzibar, kwa kuwa bado ni mjumbe wa Nec (Halmashauri Kuu ya CCM), angemuomba mwenyekiti wake aitishe mkutano mkuu lijadiliwe hilo na atoe anachokiamini, hakufanya hivyo kwa sababu hakubali vyama vingi, hataki mabadiliko katika siasa anayoitumikia, ” alisema Medeye.

Aliyekuwa kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru alisema hawezi kujibizana na watu kwani anajua anachofanya.

Alisema anayo mawazo huru na akitaka kuzungumza jambo lolote atafanya hivyo kwa utashi wake na siyo kujibizana na watu waliozungumza kwa utashi wao.

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita alisema anamheshimu Membe kwa sababu amefanya naye kazi katika chama hicho tawala na kumshauri siku nyingine anapozungumza mambo kama hayo asiegemee upande mmoja.

Alisema licha ya kuwa hayo ni mawazo yake na kila mtu ana uhuru wa kuwaza na kusema anachotaka, alipaswa apime anazungumza nini na kwa manufaa ya nani.

Guninita alisema Katiba ya nchi inamruhusu mtu kuhama chama hata mara 10 alimradi huko anakokwenda atapata vitu muhimu ikiwamo malengo yake binafsi, ya chama husika na mafanikio ya Taifa.

Alisema haikuandikwa ni lazima abaki sehemu anayoamini hana malengo nayo, au asihame kutoka chama kimoja ama kingine

No comments: