Makamu wa Rais Mh. Samia Suluhu Azindua Miradi ya Maendeleo Mkoani Geita leo - LEKULE

Breaking

5 Jan 2016

Makamu wa Rais Mh. Samia Suluhu Azindua Miradi ya Maendeleo Mkoani Geita leo

MAKAMU wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu, leo Januari 5, 2016 amezindua miradi ya maendeleo katika mkoa wa Geita iliyofadhiliwa na mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kwa ushirikiano na serikali ya Tanzania.

Mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya Tshs 12Billion uliojengwa kwa ushirikiano kati ya Mgodi na serikali ambao utapunguza tatizo la maji safi na salama kwa mkoa wa Geita kwa zaidi ya asilimia 35% umezinduliwa, ambapo kwa mara ya kwanza, wananchi wa Geita wataweza kunywa maji safi na salama kutoka Ziwa Zictoria.

Tatizo la maji lilikuwa ni kero kubwa kwa wakazi wa Geita kwa miaka mingi ambapo kina mama na watoto wa kike wamekuwa ndio wakiathirika wakubwa kwa kutembea umbali mrefu ili kupata maji safi kwa matumizi ya nyumbani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Makamu wa Rais alisema “Serikali ya awamu ya tano imekusudia kuleta maendeleo ya kasi kwa Wananchi kwa kushirikiana na wadau mablimbali wa maendeleo kama inavyodhihirika katika mradi huu”

Makamu wa Rais aliweza pia kutembelea na kuzindua muendelezo wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Geita ambayo ilijengwa mwaka 1957. GGM imeweza kutoa ufadhili wa ukarabati wa majengo hayo kwa thamani ya zaidi ya shilingi 800 Milioni ambapo ukarabati umekwenda sambamba na utoaji wa vifaa adimu kwa ajili ya vipimo na matibabu ya moyo, meno nk. Hospitali hii teule inahudumia zaidi ya wagonjwa milioni 1.7 kwa mwezi.

“Ni kusudio la GGM kuona kuwa jamii inayotuzunguka inakuwa katika hali nzuri na bora kuliko hapo mwanzo kwa kuwepo kwetu hapa Tanzania. Hii ni sehemu ya kutimiza dhamira yetu hii na tunaishukuru serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wake thabiti na kwa kuweka mazingira mazuri ya utendaji” alisema Mkurugenzi Mkuu wa GGM, Terry Mulpeter.

Miradi mingine aliyoweza kutembelea na kuzindua ni mradi wa ushonaji na kutarizi ulio chini ya mradi mkubwa wa kuendeleza uchumi kwa Wananchi wa Geita uitwao Geita Economic Development Program (GEDP) ambao unahusisha miradi ya kilimo cha Mpunga na Alizeti, Kufyatua Matofali ya Interlocking blocks na Uchomeleaji utakaoweza kuleta ajira zaidi ya 300 kwa vijana wa mkoa wa Geita.
  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza jambo na Mganga Mfawidhi wa Hospitali teule ya Mkoa wa Geita, Dkt. Adam Sijaona, wakati alipofanya ziara kwenye wadi ya wagonjwa wa upasuaji ya wanaume, katika Hospitali hiyo iliyojengwa kwa ufadhili wa Kampuni ya Geita Gold Mining (GGM). PICHA ZOTE NA OTHMAN MICHUZI, GEITA.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwasalimia baadhi ya wananchi wa Mji wa Geita waliokuwepo Hospitalini hapo leo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza jambo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu (kulia) wakati wa ziara yake katika Hospitali teule ya Mkoa wa Geita, leo Januari 5, 2016. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mh. Fatma Mwassa pamoja na Mbunge wa Viti Maalum Geita Mjini, Mh. Vick Kamata.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akipokea taarifa ya Hospitali teule ya Mkoa wa Geita, kutoka kwa Mganga Mkuu wa Mkoa, Dkt. Joseph Kisala mara baada ya kuisoma. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mh. Fatma Mwassa. 
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu akizungumza na wananchi pamoja na wauguzi wa Hospitali teule ya Mkoa wa Geita. 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akipokea moja vifaa tiba vilivyokabidhiwa hospitalini hapo na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Geita Gold Mining (GGM), Terry Mulpeter, ikiwa ni sehemu ya mchango wao kwa jamii ya watu wa Geita, leo Januari 5, 2016. wengine pichani toka kulia ni Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mh. Suleiman Jaffo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mh. Fatma Mwassa, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dkt. Joseph Kisala, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu pamoja na Mganga Mfawidhi wa Hospitali teule ya Mkoa wa Geita, Dkt. Adam Sijaona.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akikabidhi vifaa hivyo kwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dkt. Joseph Kisala, mara baada ya kukabidhiwa na Uongozi wa Kampuni ya Geita Gold Mining ambao wamekuwa ni wadau wakubwa wa maendeleo ya Mkoa wa Geita.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akimkabidhi Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Geita Gold Mining (GGM), Terry Mulpeter, tuzo ya maalum ya kutambua Mchango wa Kampuni hiyo, kwa kujitoa kwake kuisaidia jamii ya watu wa Geita.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akimtishwa ndoo ya maji, Bi. Tatu Salum, Mkazi wa kijiji cha Nyankubi Mkoani Geita, mara baada ya kuuzindua mradi mkubwa wa Maji Mkoani humo leo. Nyuma yake ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mh. Gerson Lwenge.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nyankubi Mkoani Geita, mara baada ya kuuzindua mradi mkubwa wa Maji Mkoani humo leo.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mh. Gerson Lwenge, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nyankubi Mkoani Geita, mara baada ya kuuzindua mradi mkubwa wa Maji Mkoani humo leo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza jambo na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mh. Fatma Mwassa, wakati wakitoka kwenye uzinduzi wa Mradi wa Maji.
Sehemu ya wanachama wa Ushirika wa Ushonaji wa Nyakayoma wakimsikiliza Makamu wa Rais.
Mwenyekiti wa Ushirika wa Ushonaji wa Nyakayoma ambao umewawezesha vijana wa Mkoa wa Geita kujifunza na kujiajiri, Bi. Debora Mashauri akisoma risala ya ushirika huo kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan (Kulia).
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na wanaushirika huo.

Sehemu ya Mashine za ushonaji zilizotolewa na Kampuni ya Geita Gold Mining.

No comments: