Maalim Seif Afunguka Kuhusu Uchaguzi Zanzibar.......Awataka Wazanzibari Wasikubali Kuchokozwa - LEKULE

Breaking

8 Jan 2016

Maalim Seif Afunguka Kuhusu Uchaguzi Zanzibar.......Awataka Wazanzibari Wasikubali Kuchokozwa


MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema juhudi za kuutafutia ufumbuzi mkwamo wa kisiasa Zanzibar zinaendelea, na kuwataka wananchi waendelee kuwa watulivu.

Amesema katika kipindi hiki cha mazungumzo maneno mengi ya kuwavunja moyo wananchi hasa kutoka vyama vya upinzani yatasemwa, lakini amesema ufumbuzi wa tatizo hilo utapatikana kwa kuheshimu misingi ya katiba na sheria za nchi.

Maalim Seif ametoa kauli hiyo huko Hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar katika salamu zake za kuwakaribisha waumini wa dini ya Kiislamu waliohudhuria Maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW).

Amesema katika kuutafutia ufumbuzi mzozo huo, atahakikisha kuwa maamuzi ya wananchi waliyoyafanya tarehe Oktoba 25, 2015 kwa kuchagua viongozi wanaowataka yanaheshimiwa.

Ameeleza kuwa amefanya Maulid hayo ya kila mwaka huku nchi ikigubikwa na mkwamo wa kisiasa, na kusisitiza kuwa ufumbuzi wake utapatikana kwa kuzingatia matakwa ya kikatiba na sheria.

Maalim Seif ambaye ni mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Wananchi (CUF), ametoa kauli hiyo siku moja tu baada ya Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein kutamka hadharani kuwa yeye ni Rais halali wa Zanzibar kwa mujibu wa Katiba, na kuwataka wasioridhika waende mahakamani.

Aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi hatika hafla hiyo ya Maulid, na kuwataka waendeleze umoja na mshikamano wao, sambamba na kudumisha amani na utulivu. 
“Najua kuwa yatasemwa mengi katika kipindi hiki, lakini narejea wito wangu kwa wananchi kuwa msichokozeke”, alisisitiza Maalim Seif.


Hafla hiyo ya Maulid iliyoishirikisha Madrasat Nuur Islamiyya ya Ukutani Zanzibar, imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais mstaafu wa Zanzibar Dk Amani Abeid Karume, aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF Taifa Profesa Ibrahim Lipumba pamoja na Mzee Hassan Nassor Moyo.

No comments: