KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira amewataka viongozi wakuu wa Jeshi la Polisi nchini kuhakikisha wanawachukulia hatua kali askari polisi wenye tabia ya kuwabambikizia kesi wananchi.
Meja Jenerali Rwegasira alisema Jeshi hilo lina sifa nzuri nje ya nchi pamoja na hapa nchini lakini kuna baadhi ya askari wasiowaadilifu wanawaonea wananchi mitaani wasiokuwa na hatia kwa kuwabambikizia kesi ambapo wanalitia doa jeshi hilo.
“Jeshi letu lina sifa nzuri, niliwahi kwenda nchini Kenya nikaambiwa Jeshi la Polisi Tanzania lina maadili kwani hata likimkamata mhalifu linafuata sheria na utaratibu na sio kutumia nguvu kubwa kama yalivyo majeshi mengine,” alisema Rwegazira.
Rwegasira aliongeza kuwa, amefurahishwa sana na utendaji kazi wa jeshi hilo na kutaka kuongeza umakini zaidi ili kuliletea sifa zaidi jeshi hilo na yeye yupo karibu nao katika kuliendeleza jeshi hilo ili liweze kufanya kazi kwa weledi.
Alisema kuwa ni askari wachache mno wenye tabia hiyo ya kuwabambikizia kesi wananchi na kutofuata sheria za jeshi, hivyo kazi ya kupambana na askari hao inawezekana endapo viongozi wa jeshi wakiamua kulifanyia kazi.
“Utendaji kazi wenu ni mzuri, nawapongeza sana hasa mlivyosimamia uchaguzi mkuu vizuri kwani wananchi wengi walikuwa na wasiwasi kuhusu usalama wao katika kipindi cha uchaguzi, lakini mlisimama imara kuhakikisha uchaguzi unamalizika salama,” alisema Rwegasira.
Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Simba Yahya naye alitoa pongezi kwa jeshi hilo na kuwataka kuyapeleka mahitaji yao katika ofisi ya Katibu Mkuu pamoja na yeye ili waweze kuyafanyia kazi na hatimaye kuliboresha jeshi hilo.
Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi hilo nchini, IGP Ernest Mangu aliwapongeza Viongozi hao wa Wizara kwa kuwatembelea katika ofisi za Makao Makuu ya Jeshi kwani wamefarijila na kuwahakikishia viongozi hao kuwa wamejipanga vizuri katika kulinda usalama wa raia na mali zao na watayafanyia kazi maagizo waliyopewa.
Katibu Mkuu pamoja na Naibu wake wanamekamilisha ziara yao ya kuzitembelea Idara za Wizara hiyo ambazo ni Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ambapo lengo la ziara hizo ni kujitambulisha kwa viongozi hao pamoja na kujifunza kazi mbalimbali zinazofanywa na idara hizo.
No comments:
Post a Comment