Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January
Makamba, jana alitembelea maeneo ya mabondeni yaliyokumbwa na
Bomoabomoa ili kujionea hali halisi ya wananchi ilivyo.
Akizungumza mara baada ya ziara yake , January alisema kila utaratibu lazima ukumbwe na changamoto, hivyo ,safari hii, kabla ya nyumba kubomolewa, lazima kila moja ifanyiwe tathmini kwanza.
“Kila
utaratibu lazima ukumbwe na changamoto na sisi tumezibainisha na
kuzifanyia kazi, ni kweli wapo waliobomolewa lakini walipewa hati na
vibali vya ujenzi vya Serikali, ukweli ni kwamba kati ya makazi 774
yaliyokwishabomolewa ni makazi 20 tu ndiye yenye hati hizo,” alisema January.
Pia,alisema serikali imeagiza
Ofisi za Serikali za Mitaa katika maeneo yaliyobomolewa, kufanya
tathmini na kuangalia familia zinazohitaji msaada wa kibinadamu
zisaidiwe.
Hata
hivyo, alisema Serikali imebaini kuwa wananchi wengi ambao nyumba zao
zimebomolewa, takribani asilimia 70 ni wapangaji na wenye nyumba wapo
ambao walishafidiwa maeneo hayo na kuondoka, lakini baadaye wakarejea.
Alisema
katika ziara yake hiyo ya jana, kuna maeneo ya aina tatu ambayo ni
yaliyokwishabomolewa, yaliyowekwa alama ya X lakini hayajabomolewa na
yaliyo katika mazingira hatarishi, lakini hayajawekewa alama.
Alisema
katika eneo la waliowekewa alama kabla ya kubomolewa, aligundua
wananchi wengi wako katika taharuki, ingawa walikiri na kuonesha
kufahamu kuwa mazingira wanayoishi ni hatarishi.
“Nilizungumza
nao na wametaka watafutiwe maeneo mbadala lakini pia tumeona kuwa kwa
sababu wengi wao ni wapangaji, Serikali haina uwezo wa kuwatafutia
maeneo mbadala, hivyo tumewaambia wale wapangaji ni vyema wakapange
maeneo mengine salama,” alisisitiza.
Alisema
watakaowekewa utaratibu mbadala ni watakaobainika kuwa nyumba zao, zina
hati zilizotolewa na Serikali, lakini pia kupatiwa vibali vya ujenzi.
Aidha, Waziri alisema katika maeneo mengine alikotembelea, alikuta ni familia chache zilizokwishabomolewa.
Wenye hali tete
Alisema katika eneo la Mkwajuni, kulikuwa na familia nne zinazoishi katika vifusi vya nyumba zao zilizobomolewa.
“Ndio
maana nikaagiza ofisi za Serikali za Mitaa kuangalia na kutambua
familia zinazohitaji msaada wa kibinadamu zilizokumbwa na utaratibu huu
wa bomoabomoa,” alisema.
Alisisitiza
kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha nyumba hizo zinabomolewa kwa
kufuata mazingira ya kibinadamu, lakini pia alisisitiza ni lazima sheria
zifuatwe kwa kuhakikisha wanaoishi kwenye maeneo hatarishi,
wanaondolewa kabla ya kukumbwa na hatari.
Alisema
Serikali inatekeleza ubomoaji wa nyumba hizo kwa nia ya dhati ya
kuwahakikishia wananchi hao usalama, kwani katika maeneo hayo mvua kubwa
zikinyesha, maisha yatakuwa hatarini.
January
alisema katika mvua zilizonyesha mwaka 2011, takribani wakazi wa
mabondeni 49 walipoteza maisha, na mwaka huu tayari Mamlaka ya Hali ya
Hewa (TMA), ilishatangaza uwezekano wa kutokea mvua za El-nino. Alisema
ni muhimu wananchi wakahama haraka maeneo hayo.
Jambo
lingine alilosema ameshuhudia kupitia ziara hiyo ya jana, ni baadhi ya
nyumba zilizo hatarini ambazo pamoja na kutokuwepo kwa mvua, lakini
nyumba hizo ziko kwenye maeneo oevu na kuzungukwa na maji.
Nyumba
nyingine zimebainika zikitiririsha maji machafu ya chooni kwenye mito
na mabonde yanayotumika katika shughuli za kilimo cha mboga.
No comments:
Post a Comment