Siku
74 baada ya kushindwa katika Uchaguzi Mkuu mwaka jana, Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana kimefanya kikao cha kujitathmini
na kuweka mpango kazi kwa miaka mitano ijayo.
Katika
uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana, mgombea urais kwa
tiketi ya chama hicho, Edward Lowassa alishindwa na Rais John Magufuli
wa CCM aliyepata kura Milioni 8.8 sawa na asilimia 58.5.
Lowassa
alipata kura Milioni 6 sawa na asilimia 39.97 ya kura zote.Chadema pia
ilipata wabunge 70, wakiwamo 36 wa viti maalumu huku CCM ikipata wabunge
188.
Katika
chaguzi ndogo saba zilizofanyika baada ya uchaguzi huo mkuu, CCM
iliongeza wabunge takribani tisa, wakiwamo wa viti maalumu watatu na
Chadema mbunge mmoja wa kuchaguliwa.
==>Hii ni Taarifa Iliyotolewa na chama hicho jana
Katika
utaratibu wake wa kujipanga na kuendelea kutekeleza mikakati na malengo
ya muda mfupi na muda mrefu kwa ajili ya kufikia lengo kuu la kushinda
uchaguzi, kushika dola na kuongoza serikali kwa ajili ya kuwatumikia
wananchi, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekuwa na
utamaduni wa kuwa na vikao vya kujitathmini na kufanya uchambuzi kila
baada ya uchaguzi mkuu na kuweka mpango kazi unaopaswa kutekelezwa na
chama kwa miaka mitano inayofuata.
Vikao
vya namna hiyo pia vimekuwa vikifanyika kila mwanzoni mwa mwaka mpya,
lengo kubwa likiwa ni kufanya tathmini na uchambuzi wa utekelezaji wa
mpango kazi huo na kuweka mikakati ya utekelezaji wa vipaumbele kwa
mwaka husika kulingana na mpango huo.
Mapendekezo
ya vikao hivyo vya kiuchambuzi na tathmini (retreats) huwasilishwa
kwenye vikao vya kikatiba vya chama kwa ajili ya kujadiliwa na kufanyiwa
maamuzi kwa ajili ya utekelezaji wake kadri inavyoelekezwa na vikao
husika katika ngazi mbalimbali za chama.
Ni
vikao vya namna hii ambavyo huwakutanisha viongozi wa kisiasa,
watendaji na wataalam wa masuala mbalimbali, vimekuwa moja ya nguzo
muhimu za CHADEMA katika kujipanga na kuweka mikakati ya kukisuka na
kukiimarisha chama kwa ajili ya kutekeleza lengo kuu la kushika dola kwa
kuiondoa CCM madarakani na hatimaye kuwaongoza Watanzania kufikia
matamanio ya MABADILIKO YA KWELI, badala ya ‘cosmetic changes’ kama
inavyofanyika sasa chini ya CCM.
Katika
utaratibu huo huo ambao umeshakuwa ni utamaduni wa CHADEMA kwa miaka
mingi sasa, vikao hivyo vinaendelea kufanya tathmini na uchambuzi wa
mpango kazi wa mwaka 2010-2015 na kupanga kwa ajili ya 2016-2020 na
kupendekeza kwa ajili ya 2016 kabla ya kuwasilisha kwenye vikao vya
maamuzi kwa mwaka huu, ambavyo vitakaa kulingana na utaratibu wa
kikatiba.
Ufafanuzi
unaotolewa kupitia taarifa hii, utasaidia kusahihisha habari ambazo
hazina ukweli zinazolenga kupotosha umma, zinazoandikwa na baadhi ya
vyombo vya habari nchini kwa makusudi au kwa kutokujua taratibu za
CHADEMA katika kupanga na kuendesha mambo yake.
Imetolewa Alhamis, Januari 7, 2016 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA
No comments:
Post a Comment