JUMUIYA
ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inakusudia kuwafikisha wakuu wa
shule zake 15 kwenye vyombo vya sheria kutokana na madai ya ubadhirifu
wa fedha.
Akizungumza
jana jijini Dar es SaIaam, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Abdallah Bulembo
alisema zaidi ya shule 26 walizozifanyia ukaguzi, 15 zimekutwa zikiwa
na upungufu na kubwa ikiwa ni pamoja na ubadhirifu wa fedha.
“Katika
ukaguzi tulioufanya, tumebaini tatizo kubwa kwenye matumizi, watu
wamegeuza shule kuwa kichaka cha kutafuna fedha, sasa hawa tutawafikisha
kwenye vyombo vya sheria,” alisema Bulembo.
Alitoa mfano wa walimu wa shule za Tegeta, Tabata na Mwembe Tongwa ambao wameshafikishwa mahakamani kutokana na ubadhirifu.
Aidha,
Bulembo alisema taasisi yake imejizatiti katika kuhakikisha inabaki
katika soko la elimu kwa kuimarisha na kutoa elimu bora katika shule
wanazomiliki.
“
Kwa sasa Serikali imejipanga kuboresha shule zake, hivyo kutakuwa na
ushindani wa kupata wanafunzi, ili tubakie kwenye soko ni lazima
tuimarishe shule zetu,” alisema.
Bulembo
alisema pia taasisi yake imejikita katika kuanzisha vyuo mbalimbali vya
elimu ya juu kwa fani mbalimbali ikiwamo kozi ya ualimu.
Akizungumzia
ada elekezi, Bulembo alisema anaamini serikali itakuja na ada elekezi
ambayo inaendana na wakati uliopo kwani kuendesha shule kuna gharama
nyingi ambazo mzazi anachangia kupitia ada.
Serikali
pamoja na kufuta ada kwa shule inazozimiliki kuanzia shule za msingi
hadi kidato cha nne, inakusudia kuja na ada elekezi kwa shule binafsi
lengo likiwa ni kuwapunguzia mzigo wananchi.
No comments:
Post a Comment