Waziri wa Afya Atoa Mwarobaini wa Kipindupindu - LEKULE

Breaking

17 Dec 2015

Waziri wa Afya Atoa Mwarobaini wa Kipindupindu


WAZIRI wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameagiza wakuu wa mikoa, wilaya na kata kuhakikisha wanakuwa na kikosi kazi cha kupambana na kipindupindu na kutoa ripoti ya utekelezaji kwa ngazi za juu kila siku.

Mwalimu ameyasema hayo alipokuwa akiongea na wanahabari katika makao makuu ya wizara yake kuhusu namna ya kuzuia usambaaji wa mlipuko wa kipindupindu.

Amesema kuwa pamoja na kuwa na kikosi hicho, viongozi na watendaji wa mikoa na halmashauri wasimamie majukumu yao ya kukagua na kusimamia usafi katika kila kaya na kila siku ili kuboresha hali ya usafi na kuchukua hatua za kisheria kwa wanaokiuka.

Mwalimu amesema shule zote pamoja na vyuo vinavyoendelea kutoa mafunzo na taasisi mbalimbali zizingatie kanuni za afya ili kuzuia ugonjwa usiingie katika maeneo yao.

Tangu ugonjwa huu uanze jumla ya watu 11,257 walipata ugonjwa huu na kati yao jumla ya watu 177 wameshafariki ambao ni sawa na 1.5% ya waliougua.

Aidha Mwalimu alitaja mkoa ambao umekuwa na wagonjwa wengi tangu mlipuko uanze ni Dar es Salaam 4628 ambayo ni 41% ya wagonjwa wote, ikifuatiwa na Tanga 1443 ambayo ni 13%, Singida 955 ambayo ni 8%, Mwanza 841 ambayo ni 7%.

Katika mazungumzo hayo pia Mwalimu amepiga marufuku uuzaji wa matunda yaliyomenywa na chakula katika maeneo ya wazi kutokana na kuibuka kwa kasi ya ugonjwa huo.


Ameagiza pia maafisa afya kuhakikisha wauzaji wote wa vyakula wanazingatia kanuni za usafi ikiwa ni pamoja na kuosha vyombo kwa maji salama na yamoto na sabuni.

No comments: