Na Mwandishi Wetu
MTANDAO
wa Wasanii Tanzania (SHIWATA) umeamua kutekeleza kwa vitendo agizo la
Rais wa Jamhuri ya Muungano, John Magufuli la kufanya usafi nchini siku
ya sherehe za Uhuru 9/12/2015 kufagia, kulima, kuzoa taka na kusafisha
maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.
Mwenyekiti
wa SHIWATA, Cassim Taalib alisema jana Dar es Salaam kuwa usafi huo
utaanzia makao makuu yao Ilala Bungoni, soko la Ilala,Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Mmachinga Complex, Soko la Mitumba Karume,
Kariakoo, Mnazi Mmoja, Soko la Kisutu, Posta ya zamani, soko la samaki
Feri mpaka Ikulu.
Alisema
zaidi ya wanachama 300 wa SHIWATA kutoka fani mbalimbali za
wanamichezo, wasanii, waandishi wa habari na wadau wamethibitisha
kushiriki kufanya usafi huo kutokomeza ugonjwa wa kipundupindu unashika
kasi katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam.
Taalib
alisema kazi ya usafi huo itaanza saa 1.30 asubuhi kila mmoja aje na
fagio, jembe, reki, au zana yeyote ya kufanyia usafi na kuvaa mavazi
rasmi ya kufanyia kazi za usafi.
"Baada
ya kukamilisha kazi ya usafi tutamkabidhi Rais Dkt. Magufuli fagio
maalum wa Chuma kumuunga mkono katika operesheni aliyoianza ya kupambana
na mafisadi na wezi wa mali ya umma" alisema Mwenyekiti Taalib.
Alisema
fagio hilo la chuma ni mfano wa zana ambayo itamwezesha kuwafagia na
kuwatokomeza mafisadi wote hapa nchini wanajilimbikizia mali wakati
watanzania wakiishi maisha ya magumu ya mlo mmoja kwa siku.
Mwenyekiti
Taalib alisma maazimio ya kumuunga mkono Dkt. Magufuli kwa vitendo
ilifanyika Novemba 28 katika mkutano Mkuu wa mwaka wa SHIWATA
uliofanyika Dar es Salaam ambapo wanachama zaidi ya 300 waliohudhuria
kwa pamoja waliunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais wa Awamu ya Tano
kupambana na wezi wa mali ya umma.
Alisema
wasanii hao bila kujali itikadi zao kisiasa wanamuunga Dkt. Magufuli na
wameahidi kumsaidia kufichua wote wanaotuhumiwa kula fedha za umma ili
kuleta maendeleo ya kweli nchini.
SHIWATA
yenye wanachama zaidi ya 8,000 nchini wanamuunga mkono Rais Magufuli
kwa uongozi wake na wanamkaribisha kujiunga na wasanii katika kijiji cha
Mwanzega Mkuranga chenye ukubwa wa hekari 300 za makazi ambapo mpaka
sasa wamejenga nyumba 137 kati ya hizo 17 zinakabidhiwa Desemba 12,
mwaka huu.
Pia Shiwata inalo shamba la hekari 500 katika kijiji cha Ngarambe, Mkuranga ambako wanatarajia kulima mazao mbalimbali.



No comments:
Post a Comment