TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
______________________
1.0 Utangulizi
1.1
Jana, tarehe 30 Novemba, 2015, mahakama jijini London ilitoza Standard
Bank $ 32.2 milioni. Kati ya hizo $ 16.8 milioni ni faini inayolipwa kwa
Serious Fraud Office (SFO), $8.4 milioni ni “disgorgement of profits”;
na $ 7 milioni zinalipwa kwa Serikali ya Tanzania. Fedha hizo ni $ 6
milioni ambazo tulitozwa isivyostahili na $ 1 milioni ni riba ya fedha
hizo. Fedha tunazorejeshewa zililipwa isivyostahili kwa kampuni ya
Kitanzania iitwayo EGMA. Kesi inayohusika ilifunguliwa na SFO dhidi ya
Standard Bank.
1.2
Mwaka 2012/13, Serikali ya Tanzania iliamua kukopa fedha ($600 milioni)
kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Huu ni utaratibu wa
kawaida, ambapo Serikali inaingia mkataba na Benki moja (Lead arranger)
ambayo inatafuta fedha kutoka kwenye benki na taasisi nyingine za fedha.
Ni utaratibu wa kawaida pia kuwa Lead Arranger analipwa ada kwa kazi
hiyo.
1.3
Serikali ya Tanzania ilitoa kazi hiyo kwa Standard Bank, kupitia
Stanbic (T) Ltd. Fedha tulizohitaji, $600 milioni ambazo wakati huo
zilikuwa sawa na Sh.947,673,240,000.00 zilipatikana na zikatumika kama
ilivyokusudiwa. Standard Bank ililipwa asilimia 2.4 ya fedha hizo kama
ada yao. Mkopo ulikuwa na masharti ya grace period ya miaka miwili na
nusu na kulipwa kwa miaka 7 (2019).
2.0 Uchunguzi Nchini Tanzania
2.1
Mwaka 2013 kulikuwa na matatizo kwenye Stanbic Bank (T) Ltd, wakati huo
ikiongozwa na Bwana Bashir AWALE. Kwa kutumia mamlaka yake chini ya
Kifungu 47 cha Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006 na Kifungu 31 cha
Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Benki Kuu ilifanya
ukaguzi wa kulenga (Targeted Examination) benki hiyo.
2.2
Wakaguzi wa Benki Kuu, pamoja na mambo mengine, walibaini malipo
yasiyokuwa ya kawaida kuhusiana na kampuni ya Kitanzania inayoitwa EGMA.
Malipo hayo yalikuwa kinyume na taratibu za kibenki, na baadhi ya
watumishi wa Stanbic Bank (T) walishindwa kuvumilia hali hiyo. Wakaguzi
wa Benki Kuu walifuatilia malalamiko hayo na kujiridhisha kuwa uongozi
wa Stanbic Bank (T) ulifanya mambo ambayo ni kinyume na taratibu
zinazokubalika kibenki. Fedha kiasi cha $ 6 milioni kiliingizwa kwenye
akaunti ya EGMA na siku chache baadaye zilitolewa zote kwa fedha taslimu
na wala benki haikukusanya kodi ya zuio (withholding tax) kwa mujibu wa
sheria ya mapato ya kodi ya mwaka 2004 kutokana na mapato ya Standard
Bank kwa kazi ya ushauri iliyoifanya.
2.3
Kama ulivyo utaratibu, Benki Kuu ilitoa taarifa ya ukaguzi kwa
Mwenyekiti wa Bodi ya Stanbic Bank (T) Ltd na kuitaka Bodi hiyo kuchukua
hatua za kurekebisha kasoro ndani ya benki, pamoja na kutoa taarifa kwa
Financial Intelligence Unit kuhusiana na miamala yenye mashaka kwenye
akaunti ya EGMA kwa mujibu wa Sheria ya Anti-Money Laundering Act 2006.
2.4
Taarifa tulizopewa ni kuwa bodi ilikutana na kuchukua hatua
zinazostahili, ikiwemo kutoa taarifa FIU kuhusiana na miamala kwenye
akaunti ya EGMA, na kwa Wizara ya Fedha kuhusiana na kodi ya zuio.
2.5
Vile vile tumesikia kuwa bodi ya Standard Bank iliona kuwa makosa
yaliyobainishwa na wakaguzi wa Benki Kuu ya Tanzania yalistahili
kutolewa taarifa kwa SFO nchini Uingereza ambao walianzisha uchunguzi
ambao hatimaye ulipelekea kesi kufunguliwa.
3.0 Udanganyifu ulivyofanyika
3.1
Kwa taarifa zilizopo, inaelekea kuwa Standard Bank ilipanga kututoza
ada ya asilimia 1.4 tu, yaani $ 8,400,000. Hata hivyo ukafanyika ujanja
wa kudai kuwa ati anahitajika local agent wa benki hiyo, ambaye naye
alipwe asilimia 1 nyingine, na kufikisha ada yote kuwa asilimia 2.4
($14,400,000).
3.2
Local agent huyo alikuwa kampuni ya EGMA, ambayo miamala yao kuhusiana
na hizo $6,000,000 walizochukua ndiyo ilishtua wakaguzi wa Benki Kuu na
taarifa kutolewa kwa Bodi ya Stanbic (T) Ltd na hatimaye Standard Bank,
SFO na Mahakama Uingereza.
4.0 Uchunguzi Uingereza
4.1
Tarehe 29 Septemba, 2015, Mkuu wa Idara ya Rushwa kwenye SFO
aliiandikia Benki Kuu, akiomba ushirikiano wa Benki Kuu kwenye uchunguzi
na uendeshaji wa kesi dhidi ya Standard Bank Plc (ambayo sasa
inajulikana kama ICBC Standard Bank Plc).
4.2
Tarehe 29 Oktoba, 2015, Benki Kuu, iliiandikia SFO kutoa taarifa kuhusu
ukaguzi-lengwa ambao Benki Kuu iliufanya tarehe 15 – 19 Julai, 2013
kwenye Benki ya Stanbic Bank (T) Ltd. Ushahidi huo kutoka Benki Kuu
ulikuwa sehemu ya ushahidi uliosaidia SFO kushinda kesi. Katika kipindi
chote ambacho SFO ilikuwa inafanya uchunguzi, ilishirikiana na taasisi
zetu ikiwamo TAKUKURU, Benki Kuu, FIU na wengine. Mafanikio haya
yaliyopelekea kwenye uamuzi wa Tanzania kurejeshewa $ 7 milioni (Sh.15
bilioni/=) yametokana na dhamira ya kweli ya Serikali ya Uingereza na
Serikali ya Tanzania kupambana na rushwa.
5.0 Hitimisho
5.1
Tunaishukuru Serikali ya Uingereza, pamoja na SFO, kwa kuonesha njia
katika kusaidia nchi maskini zinazodhulumiwa na wapokea rushwa na watoa
rushwa. Maana zipo nchi nyingine tajiri ambazo wanapigia kelele rushwa
kwa kuangalia upande wa mpokeaji tu, na kusahau makampuni makubwa kutoka
kwao yanayopenda kuhonga watu wetu. Natoa wito kwa nchi nyingine tajiri
kutoa ushirikiano kama huu wa Serikali ya Uingereza. Nazishukuru
taasisi zetu, Benki Kuu, na TAKUKURU, FIU na wengine kwa kutimiza wajibu
wao na kutoa ushirikiano kwa SFO uliowezesha SFO kushinda kesi hii, na
sisi kurejeshewa fedha ambazo zitatumika kutatua matatizo yetu ya
maendeleo na kero za wananchi.
5.2
Baada ya ushindi huo uchunguzi unaendelea ndani ya nchi ili tujue hizo $
6 milioni zimekwenda wapi, na kama zilitumika kumhonga mtu tujue ni
nani. Katika hili tutaomba ushirikiano wa wenye kampuni hiyo ya EGMA
ambao kwa taarifa za vyombo vya habari vya Uingereza ni Bwana Harry
KITILLYA, aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Bwana
MBOYA ambaye ni marehemu na Bwana Gasper NJUU.
No comments:
Post a Comment