Namshukuru Mwenyezi Mungu aliyeiwezesha nchi yetu kutimiza miaka 54 ya uhuru kwa salama na amani.
Namshukuru Mungu pia kwa kuniwezesha kuiona siku hii nikiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Napenda kuchukua fursa hii, kuwapongeza Watanzania wenzangu kwa Taifa letu kutimiza 54 ya Uhuru tarehe 09 Desemba, 2015.
Napenda
kuwahakikishia kwamba, kama ilivyokuwa kwa Serikali za awamu
zilizopita, Serikali ya Awamu ya Tano itafanya kila lililo ndani ya
uwezo wake kuhakikisha kwamba Uhuru, Amani na Umoja na wa Taifa letu
hauchezewi na mtu, kikundi au Taifa lolote.
Tutaendelea kudumisha Uhuru wetu na Mapinduzi ya Zanzibar, tunu ambazo ni msingi wa Muungano wetu na Utanzania wetu.
Tofauti
na ilivyozoeleka tumeamua mwaka huu kusherekea kumbukumbu hizi kwa
kufanya kazi,. Wakati tunapata Uhuru Taifa letu lilikuwa likiongozwa na
kauli mbiu ya UHURU NA KAZI.
Kauli
hii ilikuwa na lengo la kuamusha moyo na uzalendo wa kufanya kazi
miongoni mwa Watanzania kwa kutambua kuwa uhuru wetu hautakuwa na maana
kama hatutafanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kujenga Taifa
linalojitegemea.
Watanzania
katika miaka ile waliitikia wito huo kwa kufanya kazi za kuwaongezea
kipato na za kujitolea katika kuunga mkono juhudi za Serikali za
kuwaletea maendeleo.
Katika
miaka ya hivi karibuni moyo na uzalendo wa kufanya kazi miongoni mwetu
umepungua sana. Kwa sababu hiyo, niliamua kutumia siku ya kumbukumbu za
uhuru wetu mwaka huu kukumbushana na kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu
ya UHURU NA KAZI kwa kufanya kazi hususan ya usafi wa mazingira.
Madhimisho ya Uhuru mwakani yatasherehekewa kama kawaida.
Nawapongeza
viongozi wa Mikoa na Wilaya na wa Taasisi za umma na binafsi na
mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyojitokeza katika kuhakikisha kuwa
zoezi la usafi wa mazingira linafanikiwa.
Napenda
kutoa wito kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinaweka mifumo na
taratibu thabiti zitakazowezesha usafi wa miji yetu kuwa endelevu.
Viongozi
wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri waache visingizio, uwezo na mamlaka ya
kuhakikisha kwamba usafi katika miji yao unadumishwa wanao. Uwezo wa
utendaji wao utapimwa pia kutokana na hali ya usafi wa miji yao.
Naomba
wananchi tushirikiane katika kuhakikisha kuwa nyumba na mazingira ya
nyumba zetu yanakuwa safi na maji ya kunywa katika maeneo ambayo
hayawekwi dawa yanachemshwa.
Aidha,
wananchi wajizuie kutupa taka ovyo na viongozi wa Serikali za mitaa,
vijiji na vitongoji wahakikishe kwamba kila nyumba inakuwa na choo.
Tutashinda vita dhidi ya maradhi kama kipindupindu ikiwa sote tutazingatia kanuni za afya. Kila mtu atimize wajibu wake.
Mwalimu alisema Uhuru na Kazi na mimi nasema Hapa Kazi Tu.
No comments:
Post a Comment