Hatua
kubwa imepigwa katika mazungumzo ya Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira
unaoendelea mjini Paris, kutafuta makubaliano ya kudumu yatakayopunguza
kasi ya mabadiliko ya tabianchi na kuyanusuru mazingira ya dunia.
Kukithiri kwa kiwango cha gesi ya Kaboni kunalaumiwa kwa ongezeko kubwa la joto duniani
Wataalamu
kutoka nchi 195 wamewasilisha rasimu ya mpango makhususi wa makubaliano
yanayonuia kuhakikisha usalama wa mazingira ya dunia kutokana na hewa
chafu inayochochea mabadiliko ya tabia nchi.
Licha ya
kukabiliwa na mapendekezo yanayokinzana, rasimu ya mpango
iliyowasilishwa mchana (05.12.2015) itaweka msingi muhimu zaidi kuwahi
kujaribiwa kuelekea makubaliano ya dunia kuhusu udhibiti wa mabadiliko
ya tabia nchi.
Jumatatu
ijayo, mawaziri kutoka kote duniani watawasili katika mji mkuu wa
Ufaransa, Paris, kuifanya rasimu hiyo kuwa makubaliano yenye uzito wa
kisheria, utakaoweka kikomo katika utoaji wa gesi ya kaboni, ambayo
hulinasa joto la jua na kusababisha ongezeko la joto katika maeneo ya
nchi kavu na baharini.
Haiwezekani, hadi itakapokuwa imefanyika
Akizungumza
baada ya kupatikana kwa mpango huo, mwakilishi wa Afrika Kusini Nozipho
Mxakato-Diseko amenukuu maneno ya marehemu Nelson Mandela, kwamba
''Mara zote kazi itaonekana kama haiwezi kufanyika, hadi pale
itakapokuwa imefanyika'', kauli ambayo imeshangiliwa mkutanoni.
Wataalamu
wameonya kuwa ongezeko hilo la joto linaweza kusababisha majanga
makubwa, yakiwemo kuongezeka kwa kina cha bahari, vimbunga na ukame wa
muda mrefu.
Kusitisha
kupanda huko kwa joto kutahitaji kusitisha matumizi ya nishati
itokanayo na makaa ya mawe, bidhaa za petroli na gesi, na pia kuacha
kuiangamiza misitu inayotunza gesi aina ya kaboni. Hayo ni mambo magumu
na yenye gharama kubwa, ambayo makampuni ya biashara hayapendi
kuyatekeleza.
Watu
maarufu duniani wapatao 50, wakiwemo nyota wa filamu na mabilionea
walifika mjini Paris, kusaidia kushawishi kupatikana kwa makubaliano ya
kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi.
Somo kutokana na mikutano iliyopita
Wataalamu
katika mkutano huo wana matumaini ya kuepuka hali iliyojitokeza katika
mkutano mwingine wa Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira uliofanyika mjini
Copenhagen mwaka 2009, ambayo yalinuia kupata makubaliano ifikapo mwaka
2012, ambayo hata hivyo yalifeli na kuvunjika.
Miaka
miwili baada ya kushindwa kwa mkutano huo wa Copenhagen, mwaka 2011,
wataalamu wa kimataifa walikutana mjini Durban na kukubaliana kupata
mpango mwingine wa kuyanusuru mazingira ya dunia.
Kwa
mujibu wa watalaamu mbali mbali, makubaliano yatakayotokana na mkutano
wa Paris yatakuwa na mapungufu ya vigezo vinavyohitajika, kuweza kuzuia
ongezeko la joto duniani kwa zaidi ya nyuzi 2, juu ya kiwango
kilichokuwepo kabla ya mapinduzi ya viwanda.
Bado kuna
tofauti kubwa kuhusu masuala muhimu, kama vile kiwango cha upunguzaji
wa hewa chafu inayochafua mazingira, upande utakaojitwisha juhumu kubwa
ya mchakato huo na muhimu zaidi, nani ataugharimia mchakato huo.
Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/ape
Mhariri: Caro Robi
Chanzo:DW
No comments:
Post a Comment