Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia
salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bi. Amina Masenza kufuatia
ajali ya basi la kampuni ya New Force kugongana na lori, na kusababisha
vifo vya watu 12, na wengine 15 kulazwa Hospitali.
Ajali
hiyo imetokea tarehe 18 Desemba, 2015 Majira ya saa nane mchana katika
Kijiji cha Mahenge, Wilaya ya Kilolo Mkoani IRINGA ambapo Basi la
kampuni ya New Force lenye namba T 483 CTF lililokuwa limebeba abiria 49
limegongana na Lori la Kampuni ya Reign-ford Limited lenye namba T 616
BEF na Tela lake lenye namba T 320 DEF lililokuwa na shehena ya mbao .
Rais
Magufuli amemuomba Mkuu huyo wa mkoa kufikisha salamu za pole kwa
familia, ndugu, jamaa na marafiki wote ambao wamepoteza ndugu zao katika
ajali hiyo mbaya
"Nimesikitishwa
sana na kutokea kwa ajali hii, ninawapa pole nyingi wote waliopoteza
ndugu zao na ninawaombea Majeruhi wote wapone haraka ili waungane na
familia zao na kuendelea na shughuli zao za maendeleo" amesema Rais
Magufuli.
Amewaombea marehemu wote kwa Mwenyezi Mungu ili azipumzishe roho zao mahali pema peponi, Amina.
Aidha
Dkt. Magufuli ametoa wito kwa watumiaji wote wa barabara hususani
madereva kuwa waangalifu waendeshapo vyombo vya usafiri na amewakumbusha
wananchi wanaotumia barabara kwa kusafiri ama kusafirisha mizigo kutoa
ushirikiano kwa vyombo husika pale wanapobaini kuwepo vitendo ambavyo ni
chanzo cha ajali.
Imetolewa na;
Gerson Msigwa,
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
18 Desemba, 2015
No comments:
Post a Comment