Shirika
la Umeme Nchini (TANESCO) limeagizwa kuhakikisha hadi kufikia tarehe 3
Januari 2016 liwe limekamilisha kufunga umeme kwenye Jengo la Ofisi za
Serikali la Mpakani mwa Tanzania na Rwanda (One Stop Border post)
lililopo eneo la Rusumo wilayani Ngara.
Agizo
hilo limetolewa jana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo alipofanya ziara kwenye Mpaka wa Tanzania na Rwanda kwa ajili ya
kukagua maendeleo ya mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa
Rusumo.
Akizungumza
katika ziara hiyo, Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Forodha cha Rusumo,
Laurent Gabriel alisema umeme kwenye jengo hilo umekuwa ukikatika mara
kwa mara na hivyo kusababisha usumbufu kwa wananchi wanaohitaji huduma
kwenye Ofisi zilizopo katika jengo hilo.
Gabriel
aliendelea kueleza kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na
matatizo ya kukatika mara kwa mara kwa umeme na pia kukosekana kwa
huduma ya mtandao wa kununua umeme kutoka nchini Rwanda.
Aidha,
Profesa Muhongo alizungumza na wananchi wanaoishi maeneo ya mpakani
hapo na walimueleza kusikitishwa kwao kuona jengo hilo linatumia umeme
kutoka nchi jirani ambao hata hivyo walisema umekuwa ukikatika mara kwa
mara na hivyo kusababisha shughuli nyingi za Serikali kukwama.
Baada
ya kuelezwa taarifa hiyo, Profesa Muhongo alisema jambo hilo
halikubaliki kwani tayari umeme wa Tanesco umefika kwenye eneo hilo
hivyo aliiagiza TANESCO kuharakisha uunganishaji wa huduma ya umeme
kwenye jengo hilo.
“Haileti
maana kutumia umeme kutoka nchini Rwanda wakati Tanesco wanao umeme
ambao tayari umefika mpakani hapa. TANESCO hakikisheni kufikia Jumapili
ijayo (tarehe 3 Januari, 2016) jengo hili liwe limeunganishwa na umeme,”
aliagiza.
Waziri
Muhongo alimuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Honorata Chitanda
kufuatilia suala hilo kwa ukaribu ili kufikia tarehe hiyo umeme uwe
umefungwa kwenye jengo hilo.
Ziara
hiyo ya Profesa Muhongo ni muendelezo wa ziara za kugagua mitambo na
miundombinu ya umeme nchini ambapo kwa sasa yupo Mkoani Kagera na huku
akiwa amekamilisha kutembelea miradi ya umeme iliyopo maeneo ya Mikoa ya
Kusini, Kaskazini, Kati na Kanda ya Ziwa.
No comments:
Post a Comment