Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akizungumza
jambo wakati wa ziara yake kwenye kituo cha kuzalisha umeme cha Kidatu.
Katikati ni Meneja wa Kituo hicho cha Kidatu, Mhandisi Justus Mtolera na
anayemfuatia ni Meneja wa Kituo cha kuzalisha umeme cha Mtera, Mhandisi
Abdallah Ikwasa.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akimsikiliza
Meneja wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Kidatu cha Mkoani Morogoro,
Mhandisi Justus Mtolera wakati wa ziara yake kituoni hapo lengo likiwa
ni kujionea uzalishaji umeme wa kituo hicho.
Bwawa la maji la kuendeshea mitambo ya kuzalisha umeme la Kidatu likionekana katika hali ya kupungukiwa na maji.
Serikali
imeagiza matoleo ya maji ya kumwagilia mashamba yanayotumia maji ya
mito inayotiririsha kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme ya Mtera na Kidatu
yafungwe.
Agizo
hilo limetolewa leo na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo alipotembelea Bwawa la Kidatu na kujionea namna ambavyo kina cha
maji kwenye bwawa hilo kilivyopungua.
Waziri
Muhongo alisema tatizo kubwa la uzalishaji mdogo wa umeme wa maji
nchini ni umwagiliaji usio zingatia taratibu za matumizi sahihi ya maji.
Alisema
mfumo wa umwagiliaji unaotumika ni wa kienyeji sio wa kitaalamu.
"Nimeshuhudia mtu anazuia maji kutiririka kwa kutumia mawe, magogo ama
viroba vya mchanga; hii sio sahihi," alisema.
Akizungumzia
umeme unaozalishwa kwa nguvu ya maji, Waziri Muhongo alisema kwa hivi
sasa ni asilimia ishirini tu inayozalishwa kutoka kwenye vyanzo vya maji
nchini.
Alisema
jumla ya uwezo wa mitambo yote ya maji (installed capacity) ni Megawati
561.84 ambapo wastani wa uzalishaji kwa sasa kutoka kwenye mitambo
hiyo ni Megawati 110 hiyo ni kuanzia tarehe 13 hadi tarehe 16 mwezi huu.
"Nimetembelea
Nyumba ya Mungu, Hale, Pangani, Mtera, Kihansi na Kidatu na kugundua
kwamba tatizo sugu ni umwagiliaji na siyo tabianchi," alisema.
Alisema mashamba ya umwagiliaji yanaongezeka Mikoani Mbeya, Iringa na Morogoro.
Aliongeza kuwa vibali vya umwagiliaji vimetolewa kienyeji bila kutafakari athari itakayotokea.
Profesa
Muhongo alisema kipindi hiki ni cha mvua hivyo wenye mashamba ya
umwagiliaji watumie maji ya mvua badala ya kuendelea kutumia mito.
Alisema
wakati mazungumzo yanaendelea, Bodi ya Maji- Bonde la Rufiji
wahakikishe wanakagua mifereji yote ya umwagiliaji inayoingiza maji
kwenye Mto wa Ruaha mkuu na kuifunga ili kuruhusu bwawa la Mtera kupata
maji.
Alieleza
kwamba kwa kufunga mifereji hiyo ndani ya siku nne hadi tano maji
yatakua yameingia kwenye bwawa la Mtera na hivyo kuweza kuendesha
mitambo.
Awali
akimueleza Waziri hali halisi ya uzalishaji umeme kwenye kituo hicho cha
Kidatu, Meneja wa Kituo, Mhandisi Justus Mtolera alisema umeme
unaozalishwa kituoni hapo kwa sasa ni megawati 50 wakati kituo hicho
kinao uwezo wa kuzalisha jumla ya megawati 204.
Mhandisi
Justus alisema kituo hicho kinayo mitambo minne ya kuzalisha umeme
lakini kutokana na tatizo la maji, mitambo miwili tu inafanya kazi
ambapo kila mmoja unazalisha kiasi cha Megawati 25.
No comments:
Post a Comment