Prof. Makame Mbarawa Aliyechukua Mikoba ya Rais Magufuli Wizara ya Ujenzi Aahidi Mazito - LEKULE

Breaking

29 Dec 2015

Prof. Makame Mbarawa Aliyechukua Mikoba ya Rais Magufuli Wizara ya Ujenzi Aahidi Mazito


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, ambaye amepokea kijiti cha Rais John Magufuli, aliyekuwa wizara hiyo kabla ya kuwania urais, amejitamba kwenda na kasi zaidi ya aliyokuwa nayo Dk. Magufuli.

“Hakuna asiyefahamu utendaji wa Rais Magufuli, na mimi nimejipanga kwenda na kasi kubwa zaidi na nitaendeleza pale alipoishia katika wizara hii yenye fursa nyingi zitakazoliwezesha taifa kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2020,” alisema Prof. Mbarawa jana baada kuapishwa.

 Alisema jambo la kwanza ni kufungua wilaya zote nchini kuwa katika mtandao wa lami.

Alisema pia barabara zaidi ya kilometa 1,860 zinatafutiwa wakandarasi ili zijengwe kwa ajili ya kufungua wilaya zote nchini.

Alisema kuhusu ahadi ya Rais Magufuli ya kujenga zaidi barabara za lami nchini, wanatarajia kutekeleza agizo hilo kwa kasi.

Alisema kwa upande wa reli kuna changamoto kubwa kutokana na wafanyabiashara kupitisha mizigo yao kupitia barabara za lami.

“Tumejipanga kufufua reli ili kupitisha mizigo pamoja na kujenga reli yenye uwezo wa ‘Standard Gauge’. Hii itasaidia  kusafirisha mizigo kwenda nchi za nje, ili kufikia uchumi wa kati lazima tuwe na reli ya kupeleka mizigo nchi nyingine,” alisema.

Alibanisha kuwa reli ya Standard Gauge alikuwa akiisikia tangu akiwa bunge na anaamini kila jambo kwa wakati wake na kwamba kwa sasa Watanzania watarajie kuwa na reli hiyo chini ya serikali hii.

Changamoto ya kuhamishwa wizara
Akizungumzia kuhamishwa wizara kwa kipindi kifupi ambacho aliteuliwa kushika nafasi ya Wizara ya Maji, alisema kwake yeye ni fursa na kwamba amejifunza mambo mengi na kufahamu vyema sekta ya maji.

Alibainisha kuwa, hakuwa kudhani kama Shirika la Majisafi na majitaka Dar es Salaam (Dawasco) lina wateja 148,000 na kwamba haamini ila ameagiza kuwa wahakikishe wanafikia wateja milioni moja.

“Kuhamishiwa wizara hii sioni kama kuna changamoto bali ni fursa kwani, kuna sekta ya mawasiliano ambayo kwa sasa iko vizuri mitandao imeenea nchini, kuhusu ujenzi na uchukuzi na kendeleza alipoishia Rais,” alisema.
 
Utendaji kazi
Prof. Mbarawa alibainisha kazi ambazo wizara hiyo itafanya kuwa ni kujenga barabara ya Daraja la Salenda kuanzia mwezi wa tatu mwakani.
 

Alisema pia kazi nyingine ni kujenga barabara za juu ‘Fly Over Ways’ eneo la Tazara ili kukabiliana na foleni za jijini Dar es Salaam.

No comments: