Prof. Lipumba na wafuasi wake 30 Waachiwa Huru na Mahakama Ya Kisutu - LEKULE

Breaking

4 Dec 2015

Prof. Lipumba na wafuasi wake 30 Waachiwa Huru na Mahakama Ya Kisutu



PROF. Ibrahim Lipumba, aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), ameachiwa huru na mahakama ya Hakim Mkazi, jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai nchini (DPP), imewasilisha hati maalum mahakamani hapo kueleza kutokuwa na dhamira ya kuendelea na mashitaka yanayomuhusu Prof. Lipumba na wenzake.

Prof. Lipumba ameachiwa huru siku tatu baada ya kukutana na John Pombe Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam. Prof. Lipumba alikutana na Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Novemba.

Mara baada ya kuwasilisha hati hiyo mahamani, Cyprian Mkeha, hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, ameamuru kufutwa kwa kesi hiyo na kuamuru kumwachia huru.

Prof. Lipumba alikuwa akitetewa mahakamani na Peter Kibatala. Wakili huyo alieleza mahakama kutokuwa na pingamizi na hatua hiyo.

Prof. Lipumba na wafuasi 30 wa chama hicho walishitakiwa kwa madai ya mkusanyiko usio halali, tarehe 22 na 27 Januari mwaka huu, wilayani Temeke.

Mkusanyiko huo ulikuwa maalum kwa ajili ya kumbukumbu ya mauaji wa 15 waliouawa Unguja na Pemba, Januari 26 na 27 mwaka 2001.

Mongoni mwa wafuasi hao, ni pamoja na Shabani Ngurangwa (56), Shabani Tano au Kasakwa (29), Shabani Polomo (40), Juma Mattar (54), Mohammed Kirungi (40), Athumani Ngumwai (40), Shaweji Mohamed Mketo (39) na Abdul Juma Kambaya (40).

No comments: