Mkuu
wa Operesheni wa Jeshi la Polisi Mkoani Arusha (ACP) Edward Balele
akifungua kikao kati ya Jeshi hilo na Taasisi za ulinzi kujadili
mustakabali wa usalama ndani ya mkoa huu. Kikao hicho kilifanyika katika
ukumbi wa Bwalo la Polisi Jijini hapa (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi
la Polisi Arusha).
Meneja
Mkuu wa Kampuni ya Ulinzi ya KK kanda ya Kaskazini Claude Herssens
akichangia mada katika kikao kilichoandaliwa na Jeshi la Polisi Mkoani
hapa na kuziusisha taasisi mbalimbali za ulinzi (Picha na Rashid Nchimbi
wa Jeshi la Polisi Arusha).
Baadhi
ya washiriki wa Taasisi za Ulinzi wakiwa wanasikiliza moja ya mada kwa
umakini ili baadae waweze kutekeleza kwa vitendo. (Picha na Rashid
Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha).
Katibu
wa TUPSE kanda ya Kaskazini Aisha Masoud akielezea umuhimu wa mikataba
baina ya waajiri na waajiriwa wa Makampuni ya Ulinzi. (Picha na Rashid
Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha).
Mkuu
wa Upelelezi ya Makosa Jinai Mkoa wa Arusha (SSP) Muliro Jumanne Muliro
akielezea athari za kuwa na waajiriwa ambao hawana sifa kwenye kazi za
ulinzi.
Mkuu
wa Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha (SSP), Mary Lugola akitoa
elimu ya Huduma bora kwa mteja kwa Makampuni ya Ulinzi (Picha na Rashid
Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha).
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la
Polisi mkoani hapa limeazimia kushirikiana na Makapuni binafsi ya Ulinzi
na taasisi za Ulinzi kutoka UN-ICTR, UNMICT, kitengo cha Ulinzi cha
B.O.T pamoja na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu katika kupeana
baadhi ya taarifa za uhalifu na wahalifu mara kwa mara kwa njia mtandao
wa kijamii wa “whatsApp”.
Hayo
yalisemwa na Mkuu wa Operesheni wa Jeshi hilo mkoani hapa (ACP) Edward
Balele wakati akifungua kikao kilichofanyika katika Bwalo la Polisi
mjini hapa alipokuwa anazungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoani
hapa mwishoni mwa wiki kati ya Jeshi hilo na wawakilishi wa Makampuni 31
ya Ulinzi, Benki Kuu Kanda ya Kaskazini, Mahakama ya Afrika ya Haki za
Kibinadamu,UN-ICTR na UNMICT.
Mkuu huyo
wa Operesheni alisema kwamba imefika wakati sasa kwa taasisi hizo kuzidi
kuimarisha mahusiano kwa ukaribu huku njia za kisasa za mawasiliano
zikitumika katika kupeana taarifa za uhalifu na pia kubadililishana
uzoefu katika masuala ya ulinzi na usalama.
Alisema
awali taarifa juu ya matukio mbalimbali sio kwamba zilikuwa hazipatikani
bali zilikuwa zinawafikia walengwa kwa mtindo wa ujumbe mfupi yaani SMS
lakini kwa kutumia mfumo wa kikundi cha “WhatsApp” ambacho kitapewa
jina maalum, taasisi hizo zitakuwa zinapata na kutoa taarifa kwa pamoja
na kila mhusika atakuwa anachangia mawazo yake huku wanachama wengine wa
kikundi hicho wakiwa wanaona ushauri wa kila mchangiaji.
Aidha mbali
na uundaji wa kundi hilo litakalotumia mtandao huo wa kijamii mbao
umeshika kasi katika mawasiliano pia aliyaomba Makampuni hayo kutoa
ushirikiano zaidi hasa kwa kutoa rasilimali vifaa pamoja na askari
katika kuelekea mwisho wa mwaka kwa nia ya kufanya doria ya pamoja hivyo
kudhibiti vitendo vya uhalifu ndani ya Mkoa wa Arusha.
Kwa upande
wake Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha (SSP) Muliro
Jumanne Muliro alisema kwamba Jeshi la Polisi na Makampuni hayo kila
chombo kikiwa kinawajibika ipasavyo katika nafasi yake mafanikio ya
kudhibiti vitendo vya uhalifu yatakuwa makubwa.
Alisema
anathamini mchango mkubwa unaotolewa na Makapuni hayo ya Ulinzi kwani
matukio mengi ya uvunjaji wa Maghala ya viwanda, Ofisi mbalimbali na
Makampuni yamepungua ukilinganisha na miaka ya nyuma kabla Makapuni hayo
ya Ulinzi kukubaliwa kisheria.
Mkuu huyo
wa Upelelezi alisema kwamba wakati wa uajiri wa askari hao wanatakiwa
waangalie mambo mablimbali ikiwemo akili ya kuweza kugundua kitu
kinachoashiria uhalifu, kuwa mwaminifu, kuwa mtulivu na kuwa mvumilivu
na kusema kwamba huwa anafadhaishwa sana pale anapopata shauri
linalomhusisha askari yoyote katika uhalifu hali ambayo inatia doa na
aibu kwa taasisi zote za Ulinzi.
Naye Mkuu
wa Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi
la Polisi (SSP) Mary Lugola ambaye alizungumzia juu ya huduma bora kwa
Mteja ambapo aliwataka Wawakilishi wa Makampuni hayo kuwaelekeza askari
wao kuwa, wawe na lugha nzuri kwa wateja wao jambo ambalo pengine
litakuwa linazidi kuwavutia wengine na hatimaye kupata malindo mengi
ambayo yatawaongezea kipato, mbali na hilo pia aliwataka kutotumia nguvu
kupita kiasi katika ukamataji ili kupunguza madhara makubwa yanayoweza
kutokea.
Kwa upande
wake Mkuu wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) Mkoa wa Arusha (SSP)
Ramadhani Giro yeye aliyataka makampuni hayo kufanya mazoezi ya mara kwa
mara na alisema baadhi ya Makampuni ya Ulinzi huwa yanapata mafunzo
mbalimbali kama vile matumizi sahihi ya silaha, ukakamavu na mbinu
mbalimbali za kuweza kubaini uhalifu na wahalifu toka kwa askari waliopo
katika kikosi hicho na kutoa wito kwa askari wa makapuni mengine
kujitokeza ili waweze kupata mafunzo hayo na kupunguza madhara
yanayoweza kutokea huko mbeleni.
Wakichangia
katika kikao hicho baadhi ya wawakilishi wa Makampuni ya Ulinzi,
Mwakilishi toka Kampuni ya KK Security ambaye pia ni Meneja Mkuu wa
mikoa ya Kanda ya Kaskazini Bw. Claude Herssens alilisifu Jeshi la
Polisi mkoani hapa kwa kuitikia wito kwa haraka pindi wanapoomba msaada
na kuongeza kwamba mtandao huo utawasaidia sana na hivyo kuwafanya wajue
tukio ambalo wanatakiwa kwenda kutoa msaada nje ya mipaka yao ya kazi
na tukio ambalo litakuwa linawahusu Polisi pekee.
Naye Katibu
wa Chama Cha waajiriwa wa Makampuni Binafsi Kanda ya Kaskazini (TUPSE)
Aisha Masoud alizidi kusisitiza kwamba bado baadhi ya Kampuni hizo
zinachangamoto hasa katika suala zima la mishahara ya wafanyakazi wao
japokuwa serikali toka mwaka 2013 mwezi Agosti ilishatangaza mishahara
mipya lakini baadhi yao hawajatekeleza hilo na kuwataka wafanye hivyo
pamoja na kuwaingiza katika mifuko ya Jamii.
Mara kwa
mara Jeshi la Polisi Mkoani hapa limekuwa likifanya vikao na Makapuni ya
Ulinzi lengo likiwa ni kukumbushana majukumu ya utendaji wa kazi za
kila siku hali ambayo inasababisha kuimarika kwa hali ya usalama.


No comments:
Post a Comment