Mwenyekiti
wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa CCM wilaya ya Arusha, Vicky
Mollel ametangaza kukihama chama hicho na kuhamia Chadema.
Akizungumzia
uamuzi wake, Vicky ameeleza kuwa amechukua uamuzi huo baada ya kuchoka
na majungu yaliyo ndani ya chama hicho ambayo amedai kuwa yanasababisha
kuishi kwa kuogopa watu fulani badala ya kufuata katiba.
“Nilipokaa
niliona nadhoofisha kipaji changu kwa kumuogopa mwanadamu kwani
ninachoamini ni kuwa chama kinaongozwa na katiba na kanuni. Lakini
badala yake watu wachache wanaongoza CCM huku wakidhani siasa ni kuzusha
majungu na chuki,” Mollel aliwaambia waandishi wa habari.
Aliongeza
kuwa chama hicho hivi sasa kinatumia muda mwingi kutafuta mchawi na
nani aliyekihujumu na kwamba mwenendo huo ulimkatisha tamaa.
Mollel anatarajiwa kukabidhiwa kadi ya Chadema Jumatano wiki hii na aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho, Edward Lowassa.
Mollel
ambaye aliwahi kuwa diwani wa viti maalum, alimtaka Godbless Lema
(Mgombea ubunge kupitia Chadema) kusahau tofauti zilizokuwepo kati yao
huku akieleza kuwa hakuna urafiki wala uadui wa kudumu katika siasa.
Pia, aliwashukuru akina mama na wafuasi wa CCM waliokuwa wanamuunga mkono huku akiwaomba wamfuate Chadema.
No comments:
Post a Comment