Waziri
wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema Rais amempa kazi ya
kuhakikisha anakamilisha mchakato wa Katiba Mpya pamoja na uanzishwaji
wa Mahakama ya Rushwa.
Kura
ya Maoni ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa ilipangwa kufanyika Aprili
30, lakini Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikatangaza kuiahirisha hadi
itakapotangazwa tema, ikisema inataka kukamilisha kwanza uandikishaji
wapigakura kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25.
Lakini
kabla ya kutangaza kuahirisha kazi hiyo, vyama vya upinzani, ambavyo
vilisusia Bunge la Katiba kwa madai kuwa lilikiuka utashi wa wananchi
kwa kuweka kando sehemu kubwa ya mapendekezo yaliyokuwa kwenye Rasimu ya
Katiba, walikuwa wakitaka mchakato huo uanze upya.
Lakini
jana, Dk Mwakyembe alisema moja ya majukumu aliyopewa ni kuhakikisha
anakamilisha mchakato huo wa kuunda Katiba Mpya ulioanza miaka mitatu
iliyopita wakati Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete
alipotangaza kuanza rasmi kuwa Serikali itaanza kazi ya kuandika Katiba
Mpya.
“Kuna
masuala mengi ambayo wizara yangu inahusika nayo, mengine bado
sijayaelewa vyema kwamba yapo kwenye hatua gani, lakini suala la Katiba
Mpya hilo ni jukumu ambalo hata Rais alinitamkia kuwa amenikabidhi
niliendeleze kwa hatua iliyobaki,” alisema Dk Mwakyembe.
Kauli
yake Dk Mwakyembe ambaye amebobea kwenye sheria, haikupokelewa vizuri
na wanasiasa wa upinzani ambao walisema kutekelezwa kwa mpango huo
kutakuwa ni kuanzisha tena mgogoro bila ya sababu za maana, na kwamba
upatikanaji wa kura za Wazanzibari walioko Bara bado haujapatiwa
ufumbuzi.
Akizungumzia
tamko hilo la Dk Mwakyembe, mwanasheria mkuu wa Chadema, Tundu Lissu
alisema ikiwa Serikali inataka kuendeleza mchakato wa Katiba, ikubali
kuunda upya Bunge la Katiba kwa mujibu wa sheria.
“Sheria
ya Kura ya Maoni haina utaratibu wa kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya
na hairuhusu kupata tarehe mpya ya kupiga kura ya maoni baada ya
kuahirisha upigaji kura,” alisema mwanasheria huyo wa kujitegemea.
“Kama Mwakyembe ataendeleza upya mchakato huu, aanzie alipoishia Jaji (Joseph) Warioba.”
Bunge
la Katiba liliingia dosari baada ya wajumbe kutoka vyama vinne vya
Chadema, NLD, CUF na NCCR-Mageuzi na wengine kutoka taasisi tofauti,
kususia vikao wakidai kuwa mapendekezo ya wananchi yaliyokuwa kwenye
Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Katiba, ambayo iliongozwa na
Jaji Joseph Warioba, yalitupwa na badala yake yakawekwa mapendekezo ya
CCM.
Wajumbe
hao walitoka wakati Bunge la Katiba likiwa limekwama kwenye Sura ya
Kwanza na ya Sita zinazozungumzia Muundo wa Muungano, baada ya Tume ya
Warioba kuwasilisha mapendekezo yanayotaka serikali tatu, huku wajumbe
wengi wa chombo waliotoka CCM wakitaka uendelee muundo wa sasa wa
serikali mbili.
Pamoja
na wajumbe wa vyama hivyo vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) kujiengua, Bunge la Katiba liliendelea na mchakato na kufikia
kupitisha Katiba inayopendekezwa ambayo ingepigiwa kura na wananchi
Aprili 30, lakini haikuwezekana.
No comments:
Post a Comment