POLISI
mkoani Arusha imewatia mbaroni watu wawili wanaohusishwa na tukio la
kuuawa kinyama kwa kuchinjwa shingo kwa Mkuu wa Idara ya Upelelezi ya
Ulinzi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Stephen Kisamo.
Kifo
cha Kisamo kinahusishwa na mambo mengi yakiwemo vita ya kupambana na
ujangili, ikielezwa mkuu huyo alikuwa na siri nzito juu ya watu
wanaojihusisha na ujangili wakiwemo wafanyabiashara wakubwa wa ndani na
nje ya Arusha, watumishi wa serikali na wanasiasa.
Habari
kutoka ndani ya Jeshi la Polisi Arusha zilieleza tayari imewatia ndani
watu wawili ambao ni marafiki wakubwa wa Kisamo na wanajua siri nzito
kutokana na kunaswa kwa mawasiliano ya simu ya kiganjani kati ya
marehemu na watu fulani muda mfupi kabla ya mauti kumfika ambao polisi
inawachunguza kwa karibu.
“Wasiliana
na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas sisi tumeshakamata
watu wawili wa karibu na marehemu na sms na mawasiliano yanatia shaka,
lakini ukweli utajulikana muda si mrefu,” kilieleza chanzo chetu cha
habari ndani ya Jeshi la Polisi.
Kamanda
Sabas alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo Desemba 18, mwaka huu
asubuhi katika eneo la Kikwakwaru jijini Arusha muda mfupi baada ya
Kisamo kutoka nyumbani kwake akiwa na gari aina ya Mazda.
Sabas
alisema siku hiyo hiyo jioni alifika kituoni hapo mke wa marehemu na
kueleza juu ya kutoweka kwa mumewe ambapo mara moja polisi walianza
kufuatilia jambo hilo bila mafanikio.
Kamanda
Sabas alisema usiku, Polisi ilipokea taarifa kutoka kwa raia wema wa
eneo hilo la Kikwakwaru kuhusu kuonekana kwa gari hilo likiwa
limeegeshwa maeneo hayo kwa muda mrefu bila kuonekana mtu yeyote ambapo
walifika na kulikuta gari hilo, lililovutwa hadi katika Kituo Kikuu cha
Polisi usiku huo na baadaye lilitambuliwa na mke wa Kisamo.
Baadaye
walirejea eneo la tukio kwa lengo la kutafuta mwili wa marehemu huyo,
lakini hawakufanikiwa kuupata mwili wala kumuona kachero huyo ambapo
walilazimika kuomba ruhusa ya kupekua gari hilo.
Alisema
baada ya kuomba ruhusa hiyo, mke wa marehemu alipowasilisha ufunguo wa
akiba wa gari na Polisi walipofungua na kuanza upekuzi walikuta mwili wa
marehemu ukiwa umekunjwa kwenye buti, huku shingo yake ikiwa imechinjwa
eneo la nyuma ya shingo yake.
Aidha,
Kamanda Sabas alisema kwa mujibu wa maelezo ya mkewe, mumewe alikuwa
mgonjwa na alikuwa akijiandaa kwa safari ya India kwa matibabu, hivyo
kabla ya tukio walidhani alitekeleza gari baada ya kuzidiwa na ugonjwa.
Mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.
No comments:
Post a Comment