SERIKALI imesema siku ya Desemba 9 iliyopangwa kuwa siku ya usafi wa mazingingira haitawafanya wafanyakazi wa utumishi wa umma kwenda kazini bali wataungana na wananchi kwenye maeneo wanayoishi kwa kufanya usafi wa mazingira.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw Assah Mwambene alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo jijin Dar es salaam na kusema kwamba Watumishi wa Umma wanatakiwa wabaki nyumbani na kufanya usafi katika maeneo yao na yale watakayo pangiwa na viongozi wa mitaa wanayoishi.
“Kila mwananchi ahakikishe eneo lake ni safi”Alisema Mwambene.
Mkurugenzi amesema kuwa Watumishi wa Umma hawataenda kazini badala yake watabaki nyumbani na kufanya usafi kwa kushirikiana na wananchi kusafisha maeneo yanayozunguka mitaa wanayoishi ikiwemo hospitali,kuzibua mitaro iliyoziba pamoja na kuzoa taka zilizolundikana sehemu ambazo sio rasmi.
Ameongeza kuwa muongozo kuhusu namna zoezi la usafi litakavyotekelezwa umeshatolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI kwa Uongozi wa Mikoa hadi Mitaa na kilichobaki ni utekelezaji tuu wa agizo hilo kwa kila mwananchi sehemu anayoishi,anayofanyia shughuli nyingine za kila siku kuhakikisha anafanya usafi.
Aidha Mkurugenzi amewataka viongozi wa kila eneo kutengeneza utaratibu mzuri ambao utafanikisha zoezi la usafi kufanikiwa kwa kuhakikisha wanasimamia kwa ukamilifu na kuwahimiza wananchi kuwa na tabia ya kusafisha maeneo wanaoishi kwa kuwa ni wajibu wao kufanya hivyo.
Hata hivyo tarehe tisa disemba kila mwaka huwa ni siku ya kusherehekea Uhuru wa Tanganyika uliopatikana miaka hamsini na nne iliyopita lakini kwa mwaka huu itaadhimishwa kwa kufanya usafi nchi nzima.
No comments:
Post a Comment