Naibu
Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana,
Anthony Mavunde amebaini kuwepo kwa wafanyakazi wa kigeni, walioletwa
na kampuni za simu za mkononi kufanya kazi zinazoweza kufanywa na
Watanzania ikiwemo kufunga meza na viti vya kukalia.
Aidha,
amebaini kuwepo kwa baadhi ya wafanyakazi wa Kampuni ya simu ya
Halotel, raia wa Vietnam, ambao wanaishi nchini bila kibali cha kazi
wala cha kuishi. Mavunde aliyabaini hayo jana wakati alipofanya ziara ya
kukagua vibali vya ajira kwa wageni, baada ya tangazo lililotolewa na
Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na
Walemavu, Jenista Mhagama.
Akiwa
katika kampuni hiyo ya Halotel, Mavunde alibaini kuwepo kwa baadhi ya
mapungufu, ikiwemo baadhi ya wafanyakazi kutopewa mikataba ya ajira na
wenye ajira kutopewa nakala za mikataba yao.
Mavunde
aliagiza viongozi wa kampuni hiyo, kuhakikisha kufikia leo wafanyakazi
wote wanapewa mikataba huku nakala za mikataba hiyo, ikipelekwa ofisini
kwake na pia kuwataka kulipa madeni ya wafanyakazi, hasa madereva, ya
saa za ziada (overtime) haraka iwezekanavyo.
“Tumegundua
kuwepo kwa mapungufu mengi katika kampuni yenu, hii ni pamoja na
wafanyakazi wenu kutojiunga katika mifuko ya hifadhi ya jamii na
kumekuwa na makato ambayo hayapo kwa mujibu wa sheria za kazi.
"Lakini
pia kuna wageni ambao wako katika hii kampuni yenu, wanafanya kazi
ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania, kwa mfano huyu anayefunga viti,
hii kazi inafanywa na vijana wetu…kibali chake kinaisha kesho, naagiza
asipewe kingine na aondoke,” alisema Mavunde.
Aidha,
alisema katika masuala ya usalama mahali pa kazi, pia kuna mapungufu
mbalimbali, ikiwemo wafanyakazi kutopewa mafunzo ya kukabiliana na
majanga, vipimo vya afya na makosa mengine ambapo kwa mujibu wa sheria
aliwatoza faini ya Sh milioni sita.
Hata
hivyo, wakati akiendelea kutoa maagizo hayo, mmoja wa maofisa wa
Ubalozi wa Vietnam, Mai Anh Thai aliingia katika ukumbi wa mkutano na
kutaka kumkatisha Naibu Waziri kwa madai kuwa hakufuata utaratibu.
Kutokana
na kuchafuka kwa hali ya hewa huko, ilimlazimu Mshauri wa kampuni hiyo
ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, kumshauri ofisa huyo
taratibu za ukaguzi zilivyo.
Baada
ya kutoka katika kampuni hiyo, Mavunde na maofisa wa Uhamiaji, Wizara
ya Kazi, Ajira na Vijana na askari walilazimika kufika katika nyumba
ambayo iko Mikocheni, ambako inasadikiwa kuwa wapo raia wengi wa Vietnam
wanaoishi hapo, huku wengine wakiwa hawana vibali vya kuishi wala vya
kazi.
Walipofanya
msako katika nyumba hiyo, baadhi ya raia hao walijificha na kufanikiwa
kumkamata mmoja ambaye hakuwa na kibali chochote. Hata hivyo, mmoja wa
walinzi wa nyumba hiyo alisema raia hao walikuwa wengi, lakini baadhi
yao walitoroshwa juzi usiku.
Awali
akiwa katika Kampuni ya Airtel, Mavunde aliwapiga faini ya Sh milioni
nne kutokana na kuwepo na mapungufu mbalimbali katika masuala ya usalama
na afya mahali pa kazi, ambazo wanapaswa kulipa ndani ya siku 14.
Aidha,
aliwataka waajiri nchini kote, kuhakikisha wanasimamia sheria za kazi
ili kujenga nchi ambayo haina misuguano. Mavunde alionya kuwa wanaobeza
kuwa hiyo ni ‘nguvu ya soda’, wafute jambo hilo, kwani kazi hiyo ni
endelevu.
No comments:
Post a Comment