TUME
ya wataalamu waliokuwa wanakusanya maoni ya wadau wa elimu na kukokotoa
ada elekezi kwa shule za msingi na sekondari zisizo za Serikali,
wamemaliza kazi yao na tayari wamekabidhi ripoti hiyo kwa Serikali.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Sifuni
Mchome amethibitisha kukamilika kwa kazi hiyo na sasa kinachofuata ni
uchambuzi wa ripoti pamoja na kuangalia miongozo ya Serikali kabla ya
ada elekezi kutangazwa na kuanza kutumika kwa majaribio mwakani Januari.
Wataalamu
hao walipewa kazi na Serikali kuandaa ada elekezi baada ya kupata maoni
ya wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo wazazi, wananchi, wamiliki wa
shule binafsi, walimu, asasi zisizokuwa za kiserikali, taasisi
mbalimbali za umma na wadau wengine ambao wanaweza kusaidia katika
ukokotoaji huo wa ada.
Katika
ukokotoaji huo, wizara inaandaa mchanganuo wa gharama za kumsomesha
mwanafunzi kuanzia elimu ya awali, darasa la kwanza hadi kidato cha sita
kwa nia ya kutoa ada hiyo elekezi ambazo zitaendana na huduma itolewayo
kwa shule zisizo za Serikali.
Alisema
shule zitakazoteuliwa kuanza kutumika kwa ada hizo zitatangazwa pia na
wizara hiyo baada ya kukutana na wamiliki wa shule hizo na kufanya nao
mazungumzo.
Alisema majaribio hayo yatafanyika katika baadhi ya shule Tanzania nzima na sio katika baadhi ya mikoa tu.
No comments:
Post a Comment