Watu Wanne Wapandisha Kizimbani Kwa Kusambaza Taarifa za Uongo Kwenye Mtandao wa Whatsapp - LEKULE

Breaking

7 Nov 2015

Watu Wanne Wapandisha Kizimbani Kwa Kusambaza Taarifa za Uongo Kwenye Mtandao wa Whatsapp


WATU wanne wakiwemo ndugu watatu, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka ya kusambaza taarifa za uongo kwenye mtandao wa Whatsapp, kuwa nchi inaingia kwenye machafuko wakati wa uchaguzi.
 
Washtakiwa hao Leila Sinare (36), pamoja na ndugu watatu, Godfrey Soka (45), Deo Soka (40) na Monica Soka (32), walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Cyprian Mkeha.
 
Wakili wa Serikali Wankyo Simon akisaidiwa na Wakili Mwandamizi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), Johannes Kalungura, alidai kati ya Oktoba 20 na 30 mwaka huu, kupitia mtandao wa Whatsapp, Leila alisambaza ujumbe wa sauti uliokuwa na taarifa za uongo zenye lengo la kupotosha jamii.
 
Alidai ujumbe huo ulikuwa unasema “ Ndugu zangu wa kigango cha siasa, hakuna cha kutakiana uchaguzi mwema wala nini, nchi yetu inaingia kwenye machafuko muda wowote kuanzia sasa hivi na kama tulivyoambiwa nchi hii itageuka kuwa nchi ya vita, ni kweli imeingia kwenye vita.”
 
Taarifa hiyo inaeleza “maboksi yenye kura feki yamekamatwa, Jimbo la Vunjo yamekamatwa matatu, tumekamata maboksi matatu yenye kura feki Moshi mjini, maboksi sita Ilemela, Maboksi 12 Hanang, kwa kifupi uchaguzi umeshavurugika na Tanga nasikia magari yamesimama sehemu, makamanda wetu bado wanaendelea kufuatilia lakini inasemekana ni maboksi ya kura na mpaka sasa hali siyo nzuri.”
 
Aidha, taarifa hiyo inaendelea kueleza “ CCM wameingiza kura nyingi feki na niseme kutokana na hali halisi ambayo ipo hatuponi kwa sababu Mwanza vijana wameshaanza kuuawa, wameshakufa vijana wanne, watano mpaka sasa hali hiyo inaendelea…, CCM jamani tunaomba mtuachie nchi kwa amani, kweli ingelipaswa kutuua angalau kwa sumu mkabaki wenyewe, msitutese, msitutese…” 
 
Wankyo alidai, Leila alisambaza ujumbe huo wa uongo kwa lengo la kuposha jamii kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
 
Katika mashitaka mengine yanayowakabili, ndugu watatu Godfrey, Deo na Monica, alidai kati ya Oktoba 20 na 30 mwaka huu, Dar es Salaam, kwa pamoja walisambaza ujumbe huo kupitia mtandao wa Whatsapp, group la Soka, kwa lengo la kupotosha jamii kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
 

Washtakiwa walikana mashitaka na upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa. 
 
 Waliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja aliyesaini hati ya Shilingi milioni tano. Kesi imeahirishwa hadi Desemba 3 mwaka huu.

No comments: