15 Nov 2015

Watanzania tuache kufanya kazi kwa Mazoea, Rais Dk.Magufuli tembelea na huku!

mg1
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli alipotembelea kwa mara ya kwanza Wizara ya Fedha, safari ambayo ilikuwa ni ya ghafla.

[TANZANIA] Kwa sasa kila zungumzo la Mtanzania ni juu ya safari za kushtukiza za Rais wa awamu ya tano, Mh. Rais Dk. John Pombe Magufuli ambaye ameacha gumzo kwa kuanza kwa kishindo na dhana yake ya ‘Hapa Kazi Tu’!.. Kwa kutuonjesha tu,  ametembelea Wizara ya Fedha safari ya kushtukiza na kuamsha hali ya utendaji wa kazi kwa watumishi wa idara ndani ya Wizara hiyo ambapo baadhi yao hawakuwapo kwenye viti vyao kwa kile kilichoelezwa kuwa wameenda kupata chochote kitu! (Hatushangai hilo kwani tumbo nalo linahitaji kupata chochote kitu).
Dk. Mafuguli amefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya taifa Muhimbili kujionea hali ya utoaji huduma kwa wagonjwa lakini hali aliyokutana nayo nadhani majibu yake kila  mmoja anafahamu na hata sasa moja ya mashine ya kupima magonjwa makubwa inafanya kazi huku tukishuhudia Afisa habari wa idara hiyo akikadhana kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa kifaa hicho kimeanza kufanya kazi na vifaa vingine vinaendelea kushughulikiwa. (Tunapongeza kwa hilo ila tunasema kuwa Watanzania tuache kufanya kazi kwa mazoea tena mazoea ambayo yametuumiza kwa muda mrefu).
Kwa kuona umuhimu tu wa kipekee ili kufanya kazi pasipo kufuatwafuatwa ni wakati sasa Watanzania tupige kazi kwa nguvi zote kusaidia Taifa kusonga mbele.
Rais Dk. Magufuli  tunaomba pia utembelee na huku…!!! najua kila mtu atajiuliza na ‘Huku’  kuna Idara nyingi tu za Serikali zimekuwa zikishindwa kufanya kazi zake ipasavyo kisa wao ndio kila kitu katika Taifa hili?, Sasa Rais kama utapata muda unaweza ‘kuibuka’ kama wanavyosema lugha ya vijana ama kutokea ghafla hapo tu hatua chache kutoka Ikulu yetu tukufu yaani kuibukia kwa Wazee wa Bandari, yaani huku Bandarini kila mtu ni mtemi licha ya kila awamu ya uongozi kupafanyia marekebisho mahala hapo lakini mizizi yake ni mipana mno jicho la wengi ni nani ataangusha ‘mbuyu’ bandarini?.. tembelea hapo kuna madudu mengi.
Pia Rais wetu Dk. Magufuli tembelea Bohari Kuu ya Dawa (MSD) huku nako kuna tuvituvitu twingi sana kama utapata muda wewe fanya kama unapita tena unaweza kwenda hata saa 10 jioni ama saa sita mchana maana napo wamejisahau sana licha ya hapa kuwakumbusha najua hawata fumbua masikio yao.
Pia chungulia huku kwa taasisi ya Rushwa TAKUKURU nako sijui kama wamesadiki na kasi yako maana kupo kaa hakupo vile fanya kama unaenda kunywa nao chai na kujionea tuvituvitu na huenda wasiwe na hata ripoti kamili za wahusika ila watakupatia makabrasha ya watu wanaowafuatilia miaka nenda rudi.
Kama utaweza Mkuu wetu Dk. Magufuli angazia huku uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere JNIA maana nao una tuvituvitu sasa fanya kama unaenda safari ya mbali kumbe ndio unaenda kuona utendaji wao wa kazi naona nao kama wamejisahau vile maana ukiwauliza madereva teksi watakuambia pale bana pamopamo tu!!

Tunajua huku kuko kwingi ila tunakuomba pia unaweza kuwatembelea TFF maana nao wanashindwa kuisogeza mbele Taifa Stars endapo utapitia pale basi utakuwa kama umewatingisha nadhani hata Taifa Stars inaweza kuifunga Algeria katika mchezo wake wa kufuzu kombe la Dunia.. achaa nimalize na hapa kwanza Ila watanzania tuache kufanya kazi kwa mazoea.

No comments:

Post a Comment