Mwenyekiti
Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI nchini Tanzania Dkt.
Fatma Mrisho akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu Maadhimisho ya
Siku ya Ukimwi Duniani mwaka huu ambayo inaadhimishwa kwa kuwahimiza
wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya zao na kupata elimu ya
kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.
Mkurugenzi
wa Ufuatiliaji na Tathmini wa TACAIDS Dkt. Jerome Kamwela akiwaonesha
waandishi wa Habari Bango lenye Takwimu za Hali ya Maambukizi ya VVU
nchini Tanzania.
Na Nyakongo Manyama- MAELEZO.
WITO
umetolewa kwa wananchi kote nchini kuyatumia maadhimisho ya Siku ya
UKIMWI duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo Desemba 1 ya kila mwaka
kupima afya zao ili kudhibiti maambukizi mapya ya VVU.
Akizungumza
na waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam Mwenyekiti Mtendaji wa
Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI nchini Tanzania Dkt. Fatma Mrisho
amesema Siku ya Ukimwi Duniani nchini itaadhimishwa kwa kuwahimiza
wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya zao na kupata elimu ya
kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.
Ameeleza
kuwa maadhimisho ya mwaka huu yataambatana na shughuli mbalimbali
zikiwemo za Utoaji wa Elimu ya Afya na Upimaji wa hiari wa VVU katika
maeneo mbalimbali kote nchini kupitia vituo vitakavyowekwa, Kufungua
kituo cha maarifa cha udhibiti UKIMWI eneo la Manyoni mkoani Singida
ambayo ni njia kuu kuelekea mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi za Jirani za
Burundi na Rwanda.
Ameongeza
kuwa Tume kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendesha mikutano ya
kitaalam kuhusu UKIMWI, Zoezi la upimaji wa hiari wa VVU kwa wananchi,
Kupokea tamko litakalotolewa na Baraza la Watu wanaoishi na VVU pamoja
na Uzinduzi wa taarifa ya tathmini ya Sheria zinazotumika zinazohitaji
kurekebishwa zinazozuia malengo ya sifuri 3.
Aidha
Tume itapokea taarifa ya hali ya maambukizi ya VVU duniani
itakayotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon kuhusu
dunia na mapambano dhidi ya VVU.
Dkt.
Fatma amefafanua kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo anatarajiwa
kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli ambapo pamoja na mambo mengine atazindua Mfuko wa UKIMWI ambao
utakuwa chachu ya kupunguza maambukizi ya VVU nchini.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa ufuatiliaji na tathmini kuhusu UKIMWI wa
TACAIDS Dkt.Jerome Kamwela amesema kuwa kiwango cha maambukizi ya UKIMWI
kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2011/2012 kimepungua na kufikia asilimia
5.3 huku mikoa ya nyanda za juu kusini ya Njombe, Iringa na Mbeya
ikiongoza kwa kuwa na maambukizi zaidi na mikoa ya Manyara, Tanga na
Lindi ikiwa na maambukizi ya chini ya asilimia mbili.
Dkt.
Kamwela amesema kuwa maambukizi ya VVU ni mengi hasa kwa kundi la watu
wenye umri wa miaka 19-24 huku makundi ya wanaojidunga, wanaume
wanaofanya mapenzi ya jinsia moja, wanawake wanaofanya biashara ya ngono
yakiendelea kuwa katika hatari ya kuathiriwa zaidi na maambukizi ya
VVU.
No comments:
Post a Comment