Ofisi Ndogo ya Bunge jijini Dar es Salaam, imewataka wabunge wote wateule walioko majimboni kufika katika ofisi hizo Jumatano wiki hii kwa ajili ya kushiriki hafla ya kuapishwa kwa Rais Mteule itakayofanyika Novemba 5, mwaka huu katika Uwanja wa Uhuru.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu wa
Bunge, John Joel, alisema wabunge wateule watakaohudhuria hafla hiyo
wanatakiwa kuja na vyeti vya kuteuliwa walivyopewa na Wasimamizi wa
Uchaguzi.
“Kila
Mbunge mtarajiwa, atatakiwa kuwasilisha cheti kwa Maofisa wa Bunge
wakati wa mchakato wa usajili na kitambulisho kingine chochote
kinachotolewa na mamlaka inayotambulika na kinachomtambulisha jina lake
kamili kama linavyoonekana kwenye cheti cha uteuzi wa ubunge,” alisisitiza.
Aidha,
alisema mchakato wa usajili wa wabunge wateule utafanyika katika
viwanja vya Bunge la 11 na kuongeza wabunge hao watajitegemea usafiri
wa kuelekea bungeni.
Joel alisema mkutano huo utaanza siku ambayo Rais Mteule atakapoitisha Bunge.
Alisema
siku hiyo shughuli mbalimbali zitafanyika zikiwamo za uchaguzi na kiapo
kwa Spika, viapo vya wabunge, uthibitisho wa jina la Waziri Mkuu,
uchaguzi wa Naibu Spika na ufunguzi rasmi wa Bunge la 11.
Alivikumbusha
vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu vinavyotaka kusimamisha
mgombea wa nafasi ya Spika vianze mchakato wa kupata mgombea katika
ngazi ya vyama baada ya tangazo kutolewa na kuwasilisha jina lake kwa
Katibu wa Bunge.
Alivisistiza
vyama kuzingatia kuwa mgombea wa nafasi hiyo anaweza kuwa mbunge au
mwanachama yeyote wa chama hicho kwa masharti kwamba siyo mbunge mteule.
Hali
kadhalika, alisema vyama vya siasa vinatakiwa kuwasilisha jina la
mgombea Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) siku tano kabla ya uchaguzi
kujiridhisha kwamba mgombea ana sifa za kuwa mbunge.
No comments:
Post a Comment